Wanawake walia kunyimwa nafasi nyeti vyama vya siasa

28Nov 2021
Yasmine Protace
Nipashe Jumapili
Wanawake walia kunyimwa nafasi nyeti vyama vya siasa

​​​​​​​VIONGOZI wanawake kutoka vyama 19 vya siasa nchini, wamedai mfumo dume uliopo katika baadhi ya vyama vyao umekuwa ukimkandamiza mwanamke ikiwamo kutopata fursa ya ushiriki katika uamuzi.

Dk. Ave Maria Semakafu.

Hayo yalibainishwa na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa katika mafunzo ya siku tatu yaliyolenga masuala ya kijinsia katika vyama vya siasa.

Katika mafunzo hayo ambayo yaliratibiwa na Mtandao wa Jinsia (TGNP) kwa kushirikiana na Ulingo, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo walisema mfumo dume uliopo katika vyama hivyo unachangia wanawake kushindwa kupata nafasi za juu, hasa katibu au mwenyekiti.

Walisema mfumo dume uliopo katika baadhi ya vyama unachangia hata wanawake kukosa nafasi ya ushiriki katika uamuzi.

Waliiomba ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kabla ya kutoa usajili katika vyama, waonyeshwe kwanza katiba za chama kama zinamthamini mwanamke.

Hata hivyo, Dk. Ave Maria Semakafu, Mratibu wa Taifa Ulingo, alisema Sheria ya Vyama imeweka masharti kwa chama chochote kinachosajiliwa lazima kizingatie masuala ya kijinsia.

"Pamoja na kuwapo kwa sheria hiyo, bado baadhi ya vyama viongozi wa juu ni wanaume, hakuna mwanamke. Hali hiyo inachangia haya wanawake kushindwa kufanya uamuzi," alisema.

Aliongeza kuwa kuna kipengele katika katiba kinasema binadamu wote ni sawa, lakini katika hilo la usawa katika vyama linaonekana halipo.

Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, alisema wapo katika kutafakari kama viongozi wanawake wana uwakilishi katika ngazi za uongozi na kwamba tathmini ya awali inaonyesha hilo bado haijafikiwa.

Aliongeza kuwa inatakiwa kuwapo uwakilishi wa wanawake katika uongozi.

Aliongeza kuwa ilani zinasema 50 kwa 50, lakini ilani haisaidii chochote kutokana na kuwapo kwa mapengo.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa kutoka Zanzibar, Mohamed Ally Ahmed, alisema mafanikio ya usawa wa kijinsia Tanzania yatatokana na wanawake katika kupambana wenyewe.

"Sheria iboreshwe ili kuelekeza vyama kumtambua mwanamke katika nafasi za juu za uongozi," alisema.

Habari Kubwa