Wanawake wasimulia miezi miwili machungu ya corona

18Sep 2020
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanawake wasimulia miezi miwili machungu ya corona

WASHIRIKI wa semina ngazi ya jamii, wamesema kipindi cha kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 kuanzia Machi hadi Mei mwaka huu, kilikwamisha harakati za wanawake kiuchumi na kisiasa.

Mshiriki wa semina hizo mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam, Kennedy Machery, alisema harakati za mwanamke katika kujiandaa na mwaka wa uchaguzi 2020, unaweza kuleta matokeo ya ushiriki mdogo katika siasa.

Alisema pamoja na athari hizo, zipo changamoto walizokumbana nazo wanawake na wasichana kwa kukumbana na ukatili wa kijinsia.

“Mwaka wa uchaguzi kama miaka mingine, ni kawaida maandalizi ya ndani kwa ndani ya taasisi kuandaa kundi maalumu la wanawake wagombea namna ya kujipanga kukabiliana na ushindani katika siasa, ili wajiamini na kutoa hamasa kwa viongozi wanawake watarajiwa,” alisema Machery.

Alibainisha kwamba athari za maandalizi duni kwa kundi hilo kunaweza kurudisha nyuma azma ya wanasiasa, wanawake wanaoibukia.

Pia, alisema kipindi hicho baadhi ya wanawake, familia zao zilikumbwa na changamoto za kiuchumi na kusababisha baadhi ya wanawake wanaoendesha familia zao, kusambaratika.

Mwezeshaji wa semina iliyofanyika wiki hii, Agness Lukanga ambayo iliandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), alisema ipo haja ya kuongeza hamasa ya wanawake kuendelea kuinuka kiuchumi na kujenga mazoea ya kukabiliana na changamoto zozote.

“Corona ilidumaza watu biashara zao hasa wanawake, kwa nchi za Afrika, hivyo inatakiwa kutambua namna ya kujiandaa kisaikolojia na namna ya kujipanga iwapo itatokea majanga kama ya hayo duniani,” alisema Lukanga.

Mshiriki wa semina hizo kutoka Mabibo, Aloyce Anthony, alisema utamaduni wa kufuata kanuni za kiafya ikiwamo kunawa mikono iwe ni utaratibu wa kudumu.

“Kipindi cha corona ilionyesha namna watu wanavyoweza kuheshimu kanuni na taratibu, ilikuwa kila biashara, nyumba na maeneo ya taasisi za umma na binafsi unakuta utaratibu wa kunawa kabla ya kupatiwa huduma, hii ilipunguza magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu,” alisema Anthony.

Habari Kubwa