Wanawake jamii wafugaji watakiwa kuvunja ukimya

21Oct 2021
Tumaini Mafie
Arusha
Nipashe
Wanawake jamii wafugaji watakiwa kuvunja ukimya

WANAWAKE wa jamii za kifugaji katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, wameshauriwa kuvunja ukimya na kufichua vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vipigo, ndoa za utotoni, ulawiti na ubakaji ili serikali ichukue hatua ya kuwafikisha wahusika mahakamani.

Pia, wameshauriwa kukataa utamaduni wa kumaliza kesi hizo kienyeji hasa kimila, badala yake watafute haki yao kwa kuripoti kwanza matukio hayo polisi ili yafikishwe mahakamani.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Emimutie Women Organization, Rose Njilo, wakati akizungumza na wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia wilayani humo.

Alisema shirika hilo, limeamua kuvalia njuga suala la ukatili wa kijinsia hususani masuala ya ukeketaji na ndoa za utotoni unatokomezwa.

“Emimutie, tumeamua kuvalia njuga suala la ukatili wa kijinsia na tunataka kuhakikisha watoto wanasoma na kupata haki zao za msingi hususani katika jamii ya kifugaji tunapambana kuhakikisha masuala ya ukatili yanatokomezwa,” alisema Njilo.

Kabla ya kikao hicho, shirika hilo liligawa taulo za kike kwa watoto zaidi ya 300 wa shule mbalimbali za wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kufahamu kuwa wale wote watakao kaidi kupeleka watoto wao shule wajiandae kukumbana na mkono wa sheria.

“Elimu bure bado ukatae kumpeleka mtoto shule? Utaeleza kwanini umekatili agizo la serikali lakini pia nitoe rai kwa vijana wanaobaka watoto wa shule katika wilaya yangu sitafumbia macho miaka 30 itawahusu jela bila kupepesa macho,” alisema Mangwala.

Aidha, aliwataka wananchi hao kuheshimu haki za wanawake pamoja na watoto wa kike ili kuleta usawa wa kijinsia katika jamii hiyo.

Mmoja wa wakazi wa wilaya hiyo, Mariana Jacob, alisema wasichana hasa wa jamii ya kifugaji, wanalipiwa mahari wakiwa bado wadogo na hivi sasa wanalazimishwa kuolewa wakiwa bado hawajamaliza masomo.

Pamoja na mambo mengine, Shirika la Mimutie Women Organization, lilipokea cheti cha kutambua ushiriki wake katika mapambano dhidi ya ukatili kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Habari Kubwa