Wanawake kuanza kupasua ubongo

07Dec 2018
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake kuanza kupasua ubongo

KWA mara ya kwanza Tanzania imepata madaktari bingwa wanawake wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ambao wamehitimu mafunzo yao Rwanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Kitengo cha Uhusiano cha Taasisi ya Mifupa ya Moi, madaktari hao ni Dk. Aingaya Kaale na Dk. Happines Rabiel ambao wamehitimu mafunzo ya miaka sita.

Taarifa hiyo ilieleza madaktari hao wamehitimu mafunzo ya miaka sita yaliyohusisha miaka mitatu ya Shahada ya Uzamivu ya Upasuaji yaani (General Surgery) na miaka mitatu ya Shahada ya Sayansi ya Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (Msc Neurosurgery).

Taarifa hiyo ilisema hafla ya mahafali ya wahitimu hao ilifanyika Kigali chini ya usimamizi wa Chuo cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (College of Surgeons of East, Central and Southern Africa), COSECSA, ambapo Moi ni moja ya kituo cha kufundishia.

“Madaktari hawa mashujaa walipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Tiba na Afya (MUHAS), Taasisi MOI pamoja na chuo cha COSECSA,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilisema kuwa pamoja na madaktari hao wanawake kuandika historia hiyo, Tanzania imeongeza daktari bingwa mwingine, Dk. Raymond Makundi, wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, ambaye amehitimu mafunzo hayo.

“Kuhitimu kwa madaktari hao kumefanya idadi ya madaktari katika sekta hii kufikia zaidi ya kumi hapa Tanzania, madaktari bingwa wengine wawili wa upasuaji wa mifupa wa watoto wamehitimu mafunzo ya ubobezi wa juu wa upasuaji wa mifupa kwa watoto. Mabingwa hao ni Dk. Bryson Mcharo na Dk. Msami Ngowi,” ilieleza.

Katika taarifa hiyo uongozi, jumuiya na watumishi wa Moi umewapongeza mashujaa hao ambao wamepeperusha bendera ya Tanzania nchini Rwanda na kujitoa kwa kusoma kwa bidii na kufuata maelekezo ya wakufunzi.

“Ni matarajio yetu kwamba watakaporejea watatoa huduma bora na za ubobezi kwa Watanzania na kutekeleza agizo la serikali la kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana nchini,” ilieleza taarifa hiyo ya Moi.

Habari Kubwa