Wanawake Mtwara kujengewa uwezo wa kuwainua kiuchumi

21Nov 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe Jumapili
Wanawake Mtwara kujengewa uwezo wa kuwainua kiuchumi

​​​​​​​AFISA Program wa Shirika lisilo la kiserikali la Gender, linalojihusisha na utetezi wa haki za wasichana na wanawake waishio vijijini Jabir Jabir, amesema shirika hilo limedhamiria kuwajengea uwezo wanawake wa mkoa wa Mtwara ili wanufaike na mazao ya ufuta, korosho-

-na fursa nyingine za kibiashara zinazopatikana mkoani humo.

Amesema uamuzi huo umetokana na tathmini yao juu ya wanawake aliowataja kuwa ndiyo watunzani na wahudumiaji wakuu wa mazao hayo huku wengi wakiwa hawanufaiki nayo

Jabir ametoa kauli hiyo katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni na kusema kuwa jamii ikitambua na kuheshimu mchango wa wanawake katika uzalishaji mali ni wazi milango ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla itakuwa imeongezeka.

“Ni wanawake wachache wanaoweza kwenda sambamba na wanaume, kutokana na dhana ya mfumo dume tulio nao mfano hai ni hata katika uvuvi, wanaume wakishavua samaki wanamwachia mwanamke atengeneze hivyo hivyo katika korosho na ufuta, lakini uchumi wa mazao haya umetawaliwa na wanaume, tunataka sasa mwanamke nae asiachwe nyuma” amesema Jabir.

Ameongeza kuwa kupitia mradi wao wa wanawake masokoni unaotelekezwa mkoani Mtwara wenye lengo la kufanya utetezi wa haki za wanawake katika maeneo ya sokoni tayari wamewafikia wanawake zaidi ya 200 na kuwapa ujuzi,ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na wadau wengine wanaotoa mafunzo ya ujasiriamali

Ameongeza wanataka wanawake watambue haki zao katika maeneo ya biashara, elimu ya ujasiriamali, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na taasisi zinazoweza kuwawezesha kiuchumi

Amesema moja ya sababu ya kutekeleza mradi huo katika mkoa wa Mtwara ni kutokana na mwamko mkubwa wa kufanya shughuli mbali mbali za kiuchumi hivyo ni jukumu la serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwaunga mkono ili wafike mbali.

Vilevile amesema serikali mkoani Mtwara imeweka fursa mbali mbali za kiuchumi hasa katika zao la korosho ambapo jitihada mbali mbali zinafanywa katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazolikabili zao hilo la kichumi zinatatuliwa.

Kwa Upande wake Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Shadida Ndile,  kwa nafasi yake amesema kuwa wanawake wengi katika manispaa hiyo wamekuwa na mwamko mkubwa kufanya shughuli mbali mbali za kiuchumi sawa na dira ya mkoa inavyojielekeza

“Hivi karibuni Mkuu wetu wa Mkoa, Brigedia Generali Marco Gaguti alitoa dira ya mkoa hadi mwaka 2025 na kusema mkoa umedhamiria kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 162,400 hadi kufikia tani 248 msimu wa 2022/23.hivyo Utekelezaji wa mradi huu katika mkoa wa Mtwara umefika kwa wakati muafaka kwani utawahimiza wanawake kujua haki zao wanapokua sokoni ikiwemo kuepuka unyanyasaji wa kijinsia.” amesema Meya Ndile.

Habari Kubwa