Wanawake, vijana, wenye ulemavu watakiwa kujiunga kupata mikopo

21Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
Wanawake, vijana, wenye ulemavu watakiwa kujiunga kupata mikopo

DIWANI wa Masama Kusini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Cedrick Pangani, amewasisitiza wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuendelea kujiunga kwenye vikundi, ili waweze kufikiwa kwa urahisi kwenye mikopo inayotolewa na halmashauri.

DIWANI wa Masama Kusini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Cedrick Pangani.

Aliyasema hayo alipovitembelea vikundi vilivyopo ndani ya kata hiyo ambayo vinanufaika na asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Akizungumza na Kikundi cha Wajane, Wagane na Wapweke (WANA WA ASAFU), kilichopo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Makuna Pangani aliwataka wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Alisema vipo vikundi vingi vimekuwa vikipata mikopo, lakini havina elimu ya kutosha ya namna ambavyo vinaweza kuitumia mikopo hiyo kwa ajili ya kuendesha miradi ya kiuchumi, hivyo upo mkakati wa kutoa elimu ili waweze kunufaika.

“Naomba nitoe wito kwa wanufaika wa mikopo hii kuhakikisha kwamba fedha wanazopewa zinakwenda kutekeleza miradi au biashara walizokusudia na kujenga tabia ya kuzirejesha kwa wakati ili ziweze kunufaisha vikundi vingi zaidi kama inavyotarajiwa,”alisema Pangani.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuvitembelea vikundi hivyo na kutoa elimu kwa baadhi ya wanavikundi ambao hawana elimu ya kuomba mikopo ili kuwawezesha kunufaika na fedha hizo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Masama Kusini, Lilian Loth, alisema vikundi vingi vilivyopo katika kata hiyo havipendi kusajiliwa kwa kuhofia kupoteza muda wao wa kuzalisha mali na kukaa kwa ajili ya kutengeneza Katiba.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wajane, Wagane na Wapweke, Jane Massawe, alisema vikundi vingi havijapata elimu ya kuomba mikopo kutoka halmashauri na kuiomba serikali kuvitembelea vikundi vilivyopo vijijini, ili viweze kupata elimu hiyo ya mikopo.

Katibu wa kikundi hicho, Elisamia Munisi, alisema ni kabla vikundi hivyo havijapewa mikopo ni vyema vikapatiwa elimu.

Alisdema vikundi vingi vimekuwa vikikimbilia kuomba mikopo lakini hawana mradi ambao wanakwenda kuufanya jambo ambalo limekuwa likipelekea kushindwa kuirudisha mikopo hiyo.

Mtendaji wa kata ya Masama Kusini, Emanuel Simoni, alitoa wito kwa vikundi ambavyo vimefanikiwa kupata mikopo kwenye halmashauri hiyo kurejesha mikopo yao kwanza ndipo wakope tena.

Habari Kubwa