Wanawake vinara maonyesho wajasiriamali jumuiya Afrika Mashariki

05Dec 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe Jumapili
Wanawake vinara maonyesho wajasiriamali jumuiya Afrika Mashariki

ASILIMIA 60 ya washiriki wa maonyesho ya 21 ya wajasiriamali wa wadogo na Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali ni wanawake.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa, Kitila Mkumbo wakati wa ufunguzi  maonesho hayo yanayoendelea  katika uwanja wa Rock City Mall mkoani Mwanza, ambapo Prof.Mkumbo amemuakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Maonyesho hayo nyenye kauli mbiu ya " Ukuzaji ubora na ubunifu ili kuinua ushindani wa ujasiriamali wadogowadogo wa Afrika Mashariki na ahueni baada ya UVIKO-19 yameanza Desemba 2 hadi 12 mwaka huu.

Amesema mapato hayo yataenda kusaidia katika familia zao katika masuala ya chakula,matibabu na elimu ya watoto hivyo mapato hayo ni fursa ya kuvunja mnyororo wa umasikini.

Amesema asilimia 90 ya mapato ya biashara zinazofanywa na wajasiriamali wanawake yanarudi kusaidia familia na kutatua changamoto za chakula,matibabu na elimu.

Mapato hayo ni  fursa ya kuvunja umasikini na kuwapa wanawake nafasi ya kufanya biashara huku tafiti zikionesha mapato ya wanaume ni chini ya asilimia 50 na kuhoji zaidi ya asilimia 50 yanakwenda wapi.

Amesema wajasiriamali vijana  ndio matajiri wakubwa watarajiwa ambapo kwa upande wa Tanzania wamefanya utafiti wa viwanda na biashara uzalishaji bidhaa asilimia 98 unatokana na viwanda vidogo sana na vidogo. 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali wa Jumuiya ya a Afrika Mashariki Josephat Rweyemamu,amesema maonesho hayo yalianza mwaka 1999 yakiwa na washiriki 59 Sasa wameongezeka Hadi kufikia takribani wajasiriamali 1400 pia bidhaa zimeongezeka na zingine zimepata nembo za ubora.

Aidha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira Walemavu),Jenista Mhagama amesema tatizo la ajira ni kwa wote hivyo maonyesho hayo ni ufunguo wa ajira, kukuza uchumi pia ni nyenzo ya kubadilishana ujunzi ambao unaweza  kutengeneza ajira nyingi nchini pamoja na kubadilishana elimu ya ujasiliamali na kudumisha umoja na mshikamano.

Anasema maonyesho hayo yanaendana na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru  na kuonyesha  thamani ya uwepo wetu,kutumia rasilimali tulizonazo,kutumia teknolojia na ujuzi kidogo lakini tukaboresha bidhaa,ambazo zinaweza kuingia kwenye masoko makubwa ya  kimataifa.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiriamali nchini Kenya David Osiany,amesema anafarijika kuona akinamama na vijana wajasiriamali kwenye maonesho ya mwaka huu ambapo nchini Kenya sekta hiyo inachangia  asilimia 83 ya  ajira.

Amesema maonesho ya wajasiriamali yanatoa fursa kuonesha dunia kuwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki si watu wa kununua bidhaa za nje ya nchi zao bali wanao ujuzi wa kutengeneza bidhaa zenye ubora.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Robert Gabriel,amesema jumla ya wajasiriamali 1,304 wamethibitisha  ushiriki kati ya hao 794 wametoka katika nchi za Kenya,Uganda,Sudan ya Kusini,Burundi,Rwanda na 510 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema kuwa Mwanza ni eneo lenye ardhi nzuri na uchumi ,kuna maeneo mbalimbali ya uwekezaji na yakibiashara hivyo wafanyabiashara wajitokeze kuwekeza.

Aliongeza kuwa hakuna rushwa wala kuzungushana katika upatikanaji wa maeneo pia wananchi wajitokeze kwa wingi katika maonyesho hayo ili kukuza uchumi na kuzitangaza bidhaa mbalimbali za Afrika Mashariki.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara wasiwe na hofu kwani Mkoa ni salama na hali ya ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote hasa katika maonyesho hayo.

Habari Kubwa