Wanawake vinara matumizi bora simu

21Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake vinara matumizi bora simu

UTAFITI umebaini kuwa wanawake wanaomiliki simu za mkononi wanaongoza kwa matumizi mazuri ya teknolojia hiyo ikilinganishwa na wanaume.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya (REPOA), Dk. Donald Mmari, picha mtandao

Hayo yalisemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya (REPOA), Dk. Donald Mmari, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa majukumu ya teknolojia ya simu za mkononi na maendeleo.

Mmari alisema utafiti uliofanywa umeonyesha kuwa pamoja na wanawake wanaomiliki simu kuwa wachache, lakini asilimia 70 wana matumizi mazuri.

Alisema asilimia 72 ya wanaume wanamiliki simu wakiongoza kwa matumizi ya inteneti kwa asilimia 31, wakati wanawake wanaomiliki simu ni asilimia 52.

Mmari alisema wamebaini kwamba zaidi ya mawasiliano, simu inaweza kutumika katika kusaidia jamii kupata maendeleo.

"Katika miaka ya karibuni kumekuwa na mabadiliko makubwa na ubunifu kwenye kampuni za simu, ikiwamo utoaji wa huduma za kifedha, kuanzishwa kwa programu za uelimishaji wa masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi," alisema.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na GSMA ikishirikisha watafiti kutoka taasisi tatu tofauti ikiwamo REPOA, Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) na Atamizi ya Teknohama Dar es Salaam (DTBI), inabainisha kuwa simu imeleta matokeo chanya kwa watumiaji kwa kuwa zimewasaidia kuzifikia fursa mbalimbali za maendeleo.

Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mmari alisema watumiaji wa simu za mkononi wameongezeka mara tano zaidi kuanzia mwaka 2007 na walikuwa watumiaji milioni tano, sasa wamefikia milioni 25.2.

Mkuu wa tathmini wa GSMA, Kenechi Okeleke, alisema kampuni za simu nchini zimechangia ukuaji wa uchumi kutoka Dola za Marekani bilioni 2.5, mwaka 2016 na kuwa zaidi ya Dola bilioni nne mwaka 2020, ikiwa ni zaidi ya asilimia sita ya Pato la Taifa (GDP).
 
Alisema kuongezeka huko kwa uchumi kutaongeza hali ya uzalishaji kwenye kampuni za simu pamoja na kuwezesha matumuzi ya simu za mkononi chini ya mtandao mpya wa 4G.

Okeleke alisema kampuni hizo za simu ambazo zimewekeza shilingi trilioni sita katika uendeshaji wa huduma za mtandano nchini, zimechangia kwa kulipa kodi za serikali shilingi trilioni moja sawa na Dola za Marekani milioni 441.

Katika utafiti huo, Vodacom imetajwa kuwa bado ndiyo inaongoza kwa kuwa na wateja asilimia 32, ikifuatiwa na Tigo  asilimia 29, Airtel asilimia 26 na Halotel asilimia tisa, ikifuatiwa na Zantel asilimia mbili na mitandao mingine ikiwamo TTCL, Smart na Smile zote zina soko kwa asilimia moja.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DTBI, Dk. George Mulamula, alisema polisi wanajitahidi kuwatahadharisha wananchi dhidi ya wahalifu kwa njia ya mtandao ikilinganishwa na TCRA. 

Alisema polisi wamekuwa wakituma ujumbe wa maandishi kwenye simu za wananchi kuwatahadharisha kwamba wasitume fedha kwa mtu asiyemjua, wakati TCRA hawafanyi hivyo.

Dk. Mulamula alisema kampuni za simu zikiendelea na ubunifu wa kuandaa programu zinazotoa mwongozo mzuri kwa jamii zitaongeza kasi ya maendeleo.
 
"Mfano tunaweza kuleta mfumo mwingine ambao unaweza kusaidia hata mamantilie kujua jinsi alivyofanya biashara zake ili kubaini matumizi yake na faida anayoipata kutokana na biashara yake," alisema.

Habari Kubwa