Wanawake wafugaji wapewa mafunzo mabadiliko tabia nchi

08Apr 2021
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
Wanawake wafugaji wapewa mafunzo mabadiliko tabia nchi

BARAZA la Wanawake wa Kifugaji (PWC) limetoa mafunzo juu ya mabadiliko ya tabia nchi kwa wakazi wa maeneo mbalimbali wilayani Longido Mkoa wa Arusha wakiwemo wa Kijiji Cha Engusero Kata ya Noondoto Tarafa ya Kitumbeine.

Mratibu wa Mradi wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka baraza la Wanawake wa kifugaji (PWC) Grace Sikorei akitoa mafunzo kwa wakazi wa Kijiji Cha Engusero.

Mratibu wa mradi wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka katika baraza hilo, Grace Sikorei, amesema baraza hilo linatekeleza mradi huo katika wilaya tatu mkoani Arusha zikiwemo Ngorongoro,Monduli na Longido,lengo likiwa ni kuwawezesha wanawake wa jamii hizo kukabiliana na mabadiliko hayo.

Amesema mradi huo umejikita katika kuwafundisha juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji,uhifadhi wa mazingira na kutafuta njia mbadala ya kujiendeleza kiuchumi ikiwemo kujiunga kwenye vikundi vya kukopa na kuwekeza.

"Wahusika wakubwa wa mafunzo haya ni wanawake kwa sababu asilimia kubwa wao ndio waathirika wa mabadiliko ya tabia nchi kwani mabadiliko haya yanapotekea wanawake hulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji na chakula" amesema Sikorei.

Mzee wa Mila (Alaigwanani) David Shungea, amesema mabadiliko ndani ya jamii yapo ikiwemo mvua kwa sasa zimechelewa kunyesha tofauti na mwaka 2020 hali inayopelekea ukame na kusababisha mifugo kukosa chakula lakini pia mvua zinaweza kunyesha na majani yasiote.

Mzee wa mila jamii ya kifugaji (Alaigwanani) David Shungea akifuatilia mafunzo ya mabadiliko ya tabia nchi.

Habari Kubwa