Wanawake waitwa kugombea nafasi za uongozi CCM

04Jul 2019
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
Wanawake waitwa kugombea nafasi za uongozi CCM

WANAWAKE Wilayani Longido mkoani Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi  katika chaguzi za serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) mkoa wa Arusha, Musa Matoroka wakati akizundua mashina  nane ya wakereketwa wa Umoja wa  Wanawake (UWT) katika Kata ya Longido ambayo ni kata "mama" ya chadema wilayani hapa.

"Mashina haya yamejengwa makada wa CCM mbalimbali ndani ya kata ya Longido chini ya Umoja wa Wanawake (UWT) kwa hiyo niwakumbushe wananchi wa mkoa wa Arusha ambao walikuwa wamepoteza kadi zao za kupigia kura au kuhama makazi yao na ambao walikuwa hawajafikisha miaka 18 wakati wa uandiskishwaji jitokezeni kwa wingi kujiandikisha." amesema Matoroka

Amesema kuwa wanawake wana uwezo wa kuongoza sawa na wanaume hivyo ni vyema wakagombea nafasi mbalimbali za uongozi bila kuhofia mila na tamaduni za jamii ya kifugaji ambazo zinaonekana kuwa kandamizi kwa wanawake.

“Wanawake haswa mnaotoka jamii za kifugaji naomba mgombee nafasi hizi ni muhimu sana  na sisi tutawaunga mkono achaneni na dhana potofu kuwa wanaume peke yao ndiyo wanaotakiwa kugombea nafasi hizi” amesema Matoroka

Matoroka ameeleza kuwa  kila mwananchi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa hivyo ni vyema wananwake wakajitokeza kwa wingi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi tawi pamoja na nafasi za wajumbe wa serikali ya Kijiji.

Matoroka alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake kujiunga kwenye vikundi na kuvisajili ili wawze kukopa asilimia nne ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Amesema lengo la serikali la kutoa mikopo hiyo kwa wananwake,vijana na watu wenye ulemavu ni kwa sabau ni makundi muhimu katika jamii haswa katika kukuza uchumi wa familia.

" Mikopo hii inatolewa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, wanawake wanapewa asilimia 4,vijana 4 na watu wenye ulemavu  asilimia 2" alifafanua Matoroka

Kuhusu uboreshaji wa daftari la wapiga kura amesema zoezi hilo litaanza rasmi katika mkoa wa Arusha Juni 18 mwaka huu hivyo ni vyema kila mwananchi ambaye kadi yake ina tatizo au umri wake ulikuwa haujafika wakati wa uandishwaji pamoja na waliohama makazi wajakitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wapate haki ya kupiga kura katika uchaguzi ujao.

Amesema kila mwananchi ana haki ya kuchagua kiongozi hivyo ni vyema wananchi wasiokuwa na vitambulisho vya kupigia kura wakajiandikisha ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaoona wanaweza kutatua changamoto na kuharakisha maendeleo katika maeneo yao.

Awali Katibu wa CCM katika wialya hiyo, Simba  Gaddafi amesema lengo la uzinduzi wa kampeni hiyo ya longido ya kijani ni kuhakikisha CCM inachukua mitaa yote ya wilaya hiyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

"Tunaposema kampeni ya kijani siyo kuvaa nguo za kijani tuu na kupeperusha bendera,azima yetu ni kuhakikisha CCM inashinda mitaa yote katika uchaguzi wa serikali za mitaa".

Naye katibu wa UWT wilaya ya Longido Judith Laizer, amesema wanawake  wilaya ya Longido wamedhamiria kuhakikisha kuwa CCM inashinda kutokana na serikali kuwaondolea kero mbalimbali ikiwemo  maji  na huduma za Afya.

"Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kutuletea maji mradi mkubwa kutoka wilaya ya ya siha wenye thamani zaidi ya  shillingi Billion 15 na ujenzi wa hospital ya wilaya ambao unaelekea kukamilika serikali imetupa shillingi billion 1.5 na wamesema wanatuongezea shillingi million mia tano kwa ajili ya kumaliza hospital yetu" amesema Laizer