Wanawake waomba kupewa nafasi za uongozi Longido

15Sep 2021
Zanura Mollel
Longido
Nipashe
Wanawake waomba kupewa nafasi za uongozi Longido

JAMII ya kifugaji ya Masai bado haijatambua nafasi ya mwanamke katika uongozi hali inayofanya wanawake wengi wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi katika jamii hiyo kukata tamaa.

Mwenyekiti wa kitongoji Cha Kisongo kata ya Namanga. picha: zanura mollel

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kisongo, Lucy Ruben, amesema bado jamii ya Kimasai inaubaguzi katika uongozi kwa sababu wanawake hawapewi nafasi za uongozi,lakini pia hawataki kuongozwa na kabila jingine la (Ormekii).

"Hata mimi tu niliyepewa hii nafasi na wananchi wa Kisongo bado kuna wanawake wenzangu hawafurahi mimi kuwaongoza hii inakatisha tamaa, lakini tutaendelea kupambana kuhakikisha tunashika nafasi za uongozi," amesema Lucy.

Mtendaji Kata wa Namanga, Nevely Mungaya, amesema jamii ya kimaasai bado inaukiritumba wa kuona mwanamke ni mtoto hafai kuongoza, hivyo kuwanyima fursa hiyo wakati mwanamke anauwezo mkubwa wa kubeba vitu vingi.

Akielezea uongozi wa mwenyekiti Lucy amesema anajitahidi sana pamoja na kuwa kata hiyo ipo mpakani, lakini anafanyakazi kwa busara na weledi wa hali ya juu katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.

"Mimi niwaambie ndugu zangu Wamasai wawape nafasi za uongozi wakinamama kwani wanauwezo mkubwa sana katika uongozi waachane na tafsiri ya kusema hawawezi kuongozwa na mtoto (mwanamke)," amesema Mungaya.

Wilaya ya Longido Ina jumla ya vitongoji 176, vijiji 50 na kata18, lakini katika vitongoji hivyo kiongozi mwanamke ni mmoja ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Kisongo katika kata ya Namanga, huku vijiji na kata zikiongozwa na wanaume.

Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya teuzi mbalimbali akitoa fursa kwa wanawake katika nafasi za wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi na hata Mawaziri na Makatibu Wakuu, huku akiwasihi kwenda kufanya kazi kwa bidii na kujidhihirisha kuwa wanawake wanaweza wakipewa nafasi.

Katika Baraza la Mawaziri wanawake waliopata fursa ya kuongoza wizara ni Waziri wa Afya Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, Waziri wa Ulinzi Dk. Stergomena Tax, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Ashatu Kijaji.

Habari Kubwa