Wanawake waongoza vifo

24Sep 2018
Na Mwandishi Wetu
UKEREWE
Nipashe
Wanawake waongoza vifo

WAZIRI wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema hadi mazishi ya kitaifa yanafanyika, jumla ya watu 224 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na ajali ya MV. Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu.

Akitoa taarifa ya tukio zima kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye ameongoza mazishi hayo jana, akisema wanawake waliopoteza maisha jumla yao ni 126, wanaume 71, watoto wa kike ni 17 na wa kiume ni 10.

Awali, kabla ya ibada kuanza, idadi ya waliopoteza maisha ilikuwa 223, lakini mwili mmoja wa mwanamke ulipatikana mchana huu na kufanya idadi yao kufikia 224.

Alisema mipango ya serikali ya muda mrefu ni kujenga kivuko kikubwa ambacho kitakuwa kikifanya safari zake kati ya bandari ndogo ya Bugorora iliyopo kisiwa cha Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.

"Tumefanya utafiti kwenye visiwa vidogo vyote na kubaini kuna mialo zaidi ya 140. Hii itaimarishwa ili iweze kufikika na vyombo vya usafiri ambavyo ni imara," amesema.

Akitoa taarifa kuhusu tukio zima, Waziri Kamwelwe amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 20, saa 7:48 mchana na taarifa zilifikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza saa 8:10 mchana ambapo yeye na Kamati ya Ulinzi ya Usalama ya Mkoa walikimbia kuwahi eneo la tukio na kukuta watu 40 wameshaokolewa na wakazi wa kisiwa cha Ukara.

Alisema meli ya MV. Nyerere ilijengwa mwaka 2004 na kufanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 2013. "Julai mwaka huu, tulinunua injini mbili mpya na gear box zake," alisema.

Habari Kubwa