Wanawake wapaza kilio mauaji, kunyofolewa viungo

06Mar 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wanawake wapaza kilio mauaji, kunyofolewa viungo

Wanawake Shinyanga mjini wameiomba Serikali kutokemeza matukio ya mauaji dhidi yao, kwa kukatwa mapanga pamoja na kunyofolewa viungo vyao vya siri, ili waishi kwa amani na utulivu katika nchi yao.

Katibu wa umoja wa wanawake kutoka makanisa ya kiinjili Tanzania CCT manispaa ya Shinyanga Tekla Mongela akisoma risala.

Hayo yamebainishwa leo Machi 6,2020 na Katibu wa Umoja wa Makanisa ya Kiinjili Tanzania (CCT) Manispaa ya Shinyanga Tekla Mongela, wakati akisoma risala kwenye siku ya maombi ya wanawake duniani, yaliyofanyika Shinyanga mjini kwenye Kanisa la AICT Ngokolo.

Amesema changamoto kubwa ambayo inawakabili wanawake mkoani humo, ni kuwapo na matukio ya mauaji ya wanawake pamoja na kunyofolewa viungo vyao vya siri, hali ambayo imekuwa ikiwakosesha amani, na kuiomba Serikali ikomeshe matukio hayo.

“Tunaiomba Serikali itokomeze matukio ya mauaji dhidi ya wanawake pamoja na kutolewa viungo vyetu, ili tupate kuishi kwa amani katika nchi yetu, sababu mauaji haya yanatunyima amani,”amesema Mongela.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT)  Julia Selestine kutoka Buzuruga Mwanza, amewataka wanawake kuacha matukio ya ukatili majumbani mwao kwa kunyanyasa wanaume, bali wawe watii katika ndoa zao ili kuepusha vifo vya ghafla kwa waume zao na kubaki wajane.

Amesema sasa hivi wanawake wamegeuka kuwa wanyanyasaji wakubwa kwa waume zao, hasa pale wanapota fedha za vikoba na kujiona kichwa katika familia, na kuanza kutowatii wanaume na hata kuwanyima unyumba, hali ambayo imekuwa ikisababisha wanaume kufariki kwa mshituko wa moyo sababu ya kuhifadhi mambo hayo moyoni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ambaye ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye siku hiyo amesema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi ndani ya jamii, pamoja na kuwachukulia hatua waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi na kusababisha mauaji ya watu wasio na hatia.

Katika hatua nyingine Mboneko aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu, ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu wa kuchangua madiwani, wabunge na Rais, kama walivyojitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka jana.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye siku hiyo ya maombezi ya wanawake duniani mjini Shinyanga.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania KKKT Kutoka Buzuruga Jijini Mwanza Julia Selestini akitoa mahubiri kwenye maombezi hayo ya wanawake.

Habari Kubwa