Wanawake wasomba waume, watoto wao kufanyiwa tohara

10Apr 2017
Marco Maduhu
KAHAMA
Nipashe
Wanawake wasomba waume, watoto wao kufanyiwa tohara

BAADHI ya wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini wilayani Kahama, wameamua kuwachukua waume zao na watoto wao kwenda kufanyiwa tohara kwenye kampeni hiyo inayofanyika kwenye vijiji vya Mwabomba na Tumaini wilayani hapa.

vifaa vya kufanyia tohara.

Wanawake hao wamelazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na waume zao kuona aibu kutahiriwa ukubwani na hivyo kufanya muitikio wa kampeni hiyo kuwa mdogo kwa watu wazima kujitokeza kufanyiwa tohara tofauti na watoto na ambao ndio wengi wamejitokeza.

Kampeni hiyo ya kufanya tohara wilayani Kahama ilianza Machi 15, mwaka huu na inatarajiwa kuhitimishwa Aprili 11, ikiendeshwa na shirika la Intra Health International kwa lengo la kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na kansa ya shingo ya kizazi kwa wanawake ambao huathirika kwa kufanya tendo la ndoa na wanaume wasiotahiriwa.

Baadhi ya wanawake hao, Helena Gasheli, mkazi wa kijiji cha Tumaini alisema wamechukua hatua ya kuwapeleka waume zao kwa nguvu kwa kuwabeba kwenye baiskeli kwenda kufanyiwa tohara kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakigoma kutahiriwa ukubwani kwa madai ya kuogopa kuchekwa.

“Baada ya kupata elimu juu ya umuhimu wa tohara kwa mwanaume na hasa kwetu wanawake kuwa tutaepukana na kupatwa ugonjwa wa kansa ya shingo ya kizazi, nikaona nisipoteze fursa hii lazima nimpeleke mume wangu akafanyiwe tohara ili tuwe salama wote,”alisema Gasheli.

Alitoa wito kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kufanyiwa tohara badala ya kuwaachia watoto pekee kupatiwa huduma hiyo kwani ina faida kwao pamoja na kuwa na heshima katika ndoa zao kwa kuonekana wanaume rijali.

Nao baadhi ya wanaume ambao walifika kufanyiwa tohara, Ndaki Lukasi (27), ambaye amebahatika kupata watoto watatu, alikiri kuwa wapo wenzao ambao wanaona aibu kutahiriwa ukubwani na kuwataka waondoe mtazamo na wajitokeza kupewa huduma hiyo ambayo itawafanya waishi salama.

Kwa upande wake, mshauri wa ufundi wa tohara mkoani Shinyanga, Dk. Innocent Mbughi, kutoka shirika hilo la Intra Health International, alisema katika mkoa wa Shinyanga wanatarajia kutahiri wanaume 95,900 hadi kufika Septemba 30, mwaka huu na mpaka sasa wamehudumia watu 47,500 sawa na asilimia 50.

Alisema katika kampeni hiyo ambayo ina hitimishwa kesho kwenye vijiji hivyo viwili, wameshatahiri watu zaidi ya 10,000 na kwamba huduma hiyo itaendelea kutolewa kwenye vituo vyao vya kudumu 13 vilivyopo mkoa mzima ambavyo vitafanya tohara hadi Septemba 30, mwaka huu.

Habari Kubwa