Wanawake watakiwa kutokata tamaa kwenye uongozi

18Feb 2019
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanawake watakiwa kutokata tamaa kwenye uongozi

WITO umetolewa kwa wanawake, hususan vijana wanaotarajia kushika nafasi mbalimbali za uongozi, kutokata tamaa, kujiamini na kujitambua ili kutimiza malengo hayo.

Mbunge wa jimbo la Busanda, Lolensia Bukwimba.

Mbunge wa jimbo la Busanda, Lolensia Bukwimba alitoa wito huo jana wakati akichangia mada kuhusu wanawake na uongozi, misingi, maendeleo, changamoto na fursa, kwenye semina iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Alisema kuwa pamoja na kuwapo kwa changamoto miongoni mwa wanawake ikiwamo, elimu, fedha, baadhi ya mila na desturi bado fursa ipo kwa wao kuwa viongozi.

"Hivi sasa wanawake ndio viongozi wanaotarajia kwenye jamii, binafsi nilipokuwa nagombea fursa ya elimu, kujiamini, na kujitambua niliamini ninaweza kuwatumikia wananchi ingawa baadhi walisema mwanamke ataweza?," alisema Bukwimba.

Alieleza kuwa kila Mtanzania anaweza kuwa kugombea na kuwa kiongozi, bila kujali jinsia au kusubiria kuambiwa gombea nafasi fulani.

Alisema ipo mifumo dume ambayo inahitaji kuwekewa mikakati kuanzia ngazi za chini hadi vyuo vikuu ili kuwaandaa viongozi watarajiwa.

Diwani wa Kata ya Kisukuru, manispaa ya Ilala, Hellen Lyatura akielezea uzoefu wake wa uongozi kwa kipindi cha miaka minne kwenye kata hiyo, alisema mikakati ni kuboresha miundombinu, afya na elimu.

Alisema pamoja na changamoto za fedha katika kuboresha huduma za jamii, uongozi ni ubunifu ambao unabuni miradi ambayo inaweza kutatua changamoto hizo.

Habari Kubwa