Wanawake Zanzibar waungwa mkono kugombea uchaguzi mkuu

01Apr 2020
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Wanawake Zanzibar waungwa mkono kugombea uchaguzi mkuu

UWEPO wa timu ya Wanaume 10 wa mabadiliko kumeongeza uwelewa kwa jamii kuwaunga mkono wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi Mkuu.

Maelezo ya picha baadhi wanawake wa kijiji cha Bubwini kaskazini Unguja wakipatiwa elimu ya ushiriki wa wanawake kuhusu uongozi.

Akizungumza na Nipashe, Mwenyekiti wa timu hiyo Muhamed Jabir, alisema kwamba elimu waliyoitoa kuhusiana na kuwaunga mkono wanawake kugombea nafasi za uongozi kumeongeza uwelewa hasa kwa wanaume ambao walikuwa na mitazamo hasi dhidi ya wanawake kuwa viongozi.

Alisema kuwa wengi wa wanawake walikuwa wanafikiri kwamba nafasi za uongozi ni za wanaume pekee au wanawake wenye kiwango cha juu cha elimu wakati katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi zimeleza masharti ya kugombea ni kujuwa kusoma na kuandika.

“Wanawake wengi walikua na hofu kuhusu kiwango chao cha elimu kwamba hakitoshi kugombea nafasi za uongozi hasa majimboni na walikuwa wanadhani kuwa wawe na kiwango kikubwa cha elimu ikiwemo kuwa na shahada ya kwanza,Stashahada au master”alisema.

Alieleza kuwa timu ya wanaume wa mabadiliko imefanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuwaunga mkono wanawake katika harakati za uongozi hasa katika kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Alieleza kuwa wanatarajia idadi ya wanawake watakaopata nafasi za uongozi majimboni zitaongezeka na kuacha kutegemea nafasi za uteuzi.

Naye Mjumbe wa timu hiyo Dadi Kombo Maalim, alisema moja ya mafaniko waliyoyapata baadhi ya wanaume wamejitokeza kujiunga na timu hiyo ili kuweza kuongeza nguvu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu ushiriki wa mwananmke katika nafasi za uongozi.

“Wapo baadhi ya wanaume walikuwa wakaidi na hawataki kabisa kusikia mwananmke anakua kiongozi lakini sasa wanaume hao wamekua mstari wa mbele kumkubali mwanamke kuwa kiongozi”alisema Dadi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar,Faina Idarusi alisema kuwa Tume ya Uchaguzi haitambagua wala kunyanyasa mwanamke ambae atajitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi Mkuu.

“Wanawake msiogope huu ni mwaka wa uchaguzi jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi ya za uongozi ikiwemo urais,uwakilishi,udiwani na hata Ubunge ili muweze kufikia asilimia 50 kwa 50 katika vyombo vya kutunga sheria”alisema Mkurugenzi huyo.

Timu ya wanaume 10 wa mabadiliko ni miongoni mwa wanaume 20 walioteuliwa na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania Tamwa upande wa Zanzibar kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ambapo wanaume hao 10 wapo Unguja na 10 wapo Pemba.

Tamwa imekua mstari wa mbele katika kuwaunga mkono wanawake kugombea nafasi za uongozi hasa majimboni kwa kushirikiana na shirika la kimataifa kuwasaidia wanawake ulimwenguni (UN WOMEN).

Habari Kubwa