Wanja, kope bandia chanzo kikuu cha kuvimba macho

12Oct 2018
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Wanja, kope bandia chanzo kikuu cha kuvimba macho

WANAWAKE walio katika umri wa kati, wametajwa kuwa kundi linaloongoza kwa  kuvimba macho kutokana na matumizi ya bidhaa mbalimbali za urembo kama vile  wanja, kupaka rangi machoni na kubandika kope bandia.

Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Bernadetha Shilio, alisema hayo jana kwenye kilele cha Siku ya Afya ya Macho Duniani.

Dk. Shilio alisema matumizi ya bidhaa hizo kwenye macho ya binadamu,  yanachangia kwa kiasi kikubwa matatizo mbalimbali ya macho.

Alisema takwimu za mwaka jana katika hospitali mbalimbali nchini zinaonyesha kuwa kundi kubwa la wanawake walio katika umri wa kati, wanaongoza kwa matatizo ya macho kuvimba.

"Wanawake wengi walio katika umri wa kati wamekuwa ndio kinara katika tatizo la kuvimba macho ukilinganisha na wale wazee au wanaume. Hii  ni kutokana na matumizi ya vipodozi hivyo ambavyo wengi wao wamekuwa wakivitumia katika macho yao," alisema Dk. Shilio.

Kwa mujibu wa Dk. Shilio, matumizi ya vipodozi hivyo katika macho yanamuweka mtumiaji katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya macho kutokana na kemikali ambazo zimetumika katika utengenezaji wake.

"Hatari sana katika kona za jicho mtu kuweka kitu ambacho haelewi kimetengenezwa na kitu gani. Jicho linapaswa liwe safi ili kuwa na afya njema," alisema.

Aidha aliwataka wananchi kuwa na tabia ya kupima afya ya macho yao angalau mara moja kila mwaka ili waweze kutambua afya zao.

Pia alitoa onyo kwa wanachi kuacha tabia ya kutumia miwani bila kuwaona wataalam wa afya ya macho kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha kuongeza tatizo.

"Hatupaswi kuvaa miwani ya macho bila kuandikiwa na wataalamu. Lakini  pia hata matumizi ya dawa tunapaswa kuandikiwa na wataalam na si kuweka dawa katika jicho hata ile aliyoandikiwa mwenzio. Hali hii ni hatari sana kwa afya zetu,"alisema Dk. Shilio.

Mtaalamu huyo alisema hadi jana taarifa kutoka mikoa tisa zilibainisha kuwa watu 5,000 wamefanyiwa uchunguzi na 200 wamefanyiwa upasuaji.

Habari Kubwa