Wanne familia moja wafa wakiwa wamelala usiku

30Mar 2020
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Wanne familia moja wafa wakiwa wamelala usiku

WATU wanne wa familia moja katika kitongoji cha Ngilimba ‘B’ katika Kijiji cha Ngilimba Kata ya Ulowa wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wamekufa, kutokana na kuvuta hewa yenye sumu ya carbon monoxide usiku wakiwa wamelala.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, picha mtandao

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, tukio hilo lilitokea juzi saa tisa usiku.

Aidha, alisema kuwa sababu za vifo hivyo ni waliacha jiko la mkaa likiwa limewashwa ndani ya nyumba yao, kutokana na baridi iliyosababishwa na mvua kubwa kijijini hapo.

Pia Kamanda Magiligimba alisema wanafamilia hao walifunga milango yote na madirisha, hali iliyosababisha kuwapo kwa hewa ndogo ndani ya nyumba yao na kuvuta hewa ya sumu.

“Mvua ilinyesha kubwa huko Ulowa na kusababisha kuwapo kwa baridi…waliwasha jiko la mkaa na wakati wanajiandaa kwenda kulala walifunga madirisha na milango na kusababisha kuwapo kwa hewa chafu yenye sumu ambayo imesababisha kupoteza maisha yao,” alisema Magiligimba.

Aliwataja waliokufa ni Masanja Emmanuel (35), Mngole Masanja (25), Holo Masanja (5) na Matama Masanja, ambaye umri wake haukufahamika.

Alisema miili ya wanafamilia hao imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari.

Aliwataka wananchi kuacha kufunga milango na madirisha wanapokwenda kulala wala kuacha majiko ya mkaa yakiwa yamewashwa.

Habari Kubwa