Wanne kortini madai ya kughushi, kupokea rushwa

26Jan 2021
Joctan Ngelly
Geita
Nipashe
Wanne kortini madai ya kughushi, kupokea rushwa

OFISA Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na walimu watatu wa shule za msingi wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Geita wakishtakiwa kwa makosa manane ya kushawishi na kupokea rushwa na kughushi hati za mishahara.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao walighushi hati za mishahara ili waweze kujipatia mkopo kwenye benki ya Posta Sh. milioni 24.5 kitendo ambacho ni kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Washtakiwa hao ni Deogratius Kayanda (39), ambaye ni Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Paulo Matiasi (40), Mwalimu wa Shule ya Msingi Uhuru, Suzana Manyilizu (53), Mwalimu wa Shule ya Msingi Bugogo na Peter Chilangi (41), Mwalimu wa Shule ya Msingi Uhuru.

Washtakiwa wote kwa pamoja walifikishwa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Sosthenes Kiiza na waliposomewa mashtaka yao, walikana.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Kiongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Geita, Kelvin Murusuri, alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Hakimu Kiiza alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 9, mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Hakimu alisema washtakiwa wawili, Deogratius Kayanda (39) ambaye ni Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Peter Chilangi (41), Mwalimu wa Shule ya Msingi Uhuru, walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na wako mahabusu Gereza la Geita.

Alisema washtakiwa wawili Paulo Matiasi (41) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Uhuru, Suzana Manyilizu (50), Mwalimu wa Shule ya Msingi Bugogo, walitimiza masharti ya dhamana na wapo nje kwa dhamana ya mdhamini mmoja mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa kata pamoja mali isiyohamishika Sh. milioni mbili.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Kiongozi wa TAKUKURU, Mkoa wa Geita, Kelvin Murusuri, alidai kati ya Machi 1 mpaka Juni 30, 2018 maeneo ya Wilaya ya Geita, washtakiwa wote kwa pamoja walishawishi na kupokea rushwa pamoja na kughushi hati za mishahara ili waweze kujipatia mkopo.

Habari Kubwa