Wanne wa familia moja wafa katika ajali ya gari

15Jan 2023
Idda Mushi
Morogoro
Nipashe Jumapili
Wanne wa familia moja wafa katika ajali ya gari

WATU wanne wa familia moja wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori kwenye eneo la Kwambe Point A Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, akiwa amelazwa katika Kituo cha Afya St. Joseph Dumila, jana. PICHA: IDDA MUSHI

Ajali hiyo iliyotokea jana ilisababisha foleni ya magari kuanzia majira ya saa tatu asubuhi.

Ajali hiyo ilihusisha lori lenye namba za usajili T 418 DDP lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na gari ndogo aina ya Toyota Spacio lenye namba T 162 DGN ambalo.

Dereva wa lori lililohusika na ajali aliyekuwa eneo la tukio, Samir Halfan Ally alidai ajali hiyo imesababishwa na dereva wa gari dogo ambaye ni mwanamke aliyekuwa akiendesha kwa mwendo kasi na hivyo kushindwa kumkwepa.

Kwenye Kituo cha Afya St. Joseph Dumila, Mganga Mfawidhi wake, Dk. Manyele Kapongo alisema walipokea miili ya watu wanne ambao ni watu wazima wawili, binti na mtoto mdogo.

Alisema walipokea majeruhi wawili ambao ni mama na mtoto wake.

"Mmoja tumempeleka kwenye X-ray, analalamikia zaidi maumivu ya mgongo,” alisema Dk. Kapongo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga, aliyefika eneo la ajali na baadaye hospitalini, alisema tayari wametambua mwili wa mwanamke aliyekuwa akiendesha gari hilo na ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa familia hiyo na kwamba ni mtumishi wa umma.

“Tunafanya taratibu zaidi kuwasilisha ndugu, wafike kumthibitisha na kuchukua miili ya waliofariki dunia kwa ajali na sisi tunaendelea kuhakikisha majeruhi walioko hospitalini wanapata huduma ipasavyo, tunatoa pole kwa wote walioguswa na ajali hii,” alisema Mwanga.

Alitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima ambazo nyingi husababishwa na uzembe, hivyo kugharimu maisha ya watu na mali zao.

Habari Kubwa