Wanne wafa kwa kula kibudu

11Jan 2019
Ibrahim Yassin
Momba
Nipashe
Wanne wafa kwa kula kibudu

WATU wanne wa Kata ya Nzoka wilayani Momba mkoani Songwe, wamefariki dunia huku wengine 74 wakiugua baada ya kuibuka ugonjwa ambao umeelezwa kuwa ni kimeta.

Vipimo vilivyofanyika vimebaini kuwa watu hao walipatwa na mkasa huo baada ya kula kibudu cha nyama ya ng'ombe, inayosadikiwa kuwa na vimelea vya kimeta.

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Anno Maseta, alithibitisha kuwapo kwa ugonjwa huo ambao alisema uliibuka mwanzoni mwa mwezi huu baada ya watu 78 kuugua na wanne kati yao kufariki dunia.

Alisema vipimo vimebaini kuwa watu hao walifariki kwa ugonjwa wa kimeta.
 
''Ni kweli ugonjwa wa kimeta umeibuka na muda huu tuko kwenye kikao tunajadili namna ya kuudhibiti…Chanzo cha ugonjwa huu ni watu hao kula nyama ya ng'ombe aliyekufa (kibudu) akiwa na vimelea vya ugonjwa huo,'' alisema Dk. Maseta.

Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Silvester Simwinga, alisema alikula nyama hiyo iliyosababisha aanze kujisikia vibaya na alipofika katika zahanati hiyo alilazwa huku akipatiwa matibabu na baadaye alishangaa kuona wagonjwa wengine wanaongezeka.

Mgonjwa mwingine Benard Sichizya, alisema wakati anakula nyama hiyo hakujua kama ina madhara, lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda, alijikuta akizidi kuishiwa nguvu na kujisikia vibaya na ndipo alipokimbizwa katika zahanati hiyo ambako anapatiwa matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Juma Said, ambaye alithibitisha pia kuwapo kwa ugonjwa huo, alisema matokeo ya vipimo yameonyesha kuwa ugonjwa huo ni kimeta na tangu ulipoibuka kwa ugonjwa huo watu wanne walifariki kati ya 74 walioripotiwa kuugua.
 

 

Habari Kubwa