Wanne wafariki ajali ya Hiace

04Jul 2019
Salima Hamisi
LINDI
Nipashe
Wanne wafariki ajali ya Hiace

WATU wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine sita kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Hiace kuligonga lori la Kampuni ya Saruji ya Dangote.

Ajali hiyo ilitokea juzi katika kijiji cha Mto Mkavu, Tarafa ya Mchinga wilayani Lindi, barabara kuu ya Kibiti-Lindi, majira ya saa 2:00 usiku.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Sokoine mkoani hapa, baadhi ya majeruhi, Yusufu Chapuchapu, Selemani  Sabiini na Shufaa Matola, walisema wakiwa wanatoka Kilanjelanje, Wilaya ya Kilwa kwenda mjini Lindi, gari lao Toyota Hiace lililigonga lori la Dangote.

Hiace hiyo yenye namba za usajili T239 DMA iliyokuwa ikiendeshwa na Mohamed Makame, iliigonga lori hilo lenye namba T 747 DKA, lililokuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara na dereva wake akiwa anaangalia hitilafu iliyokuwa imejitokeza.

Aidha, dereva Makame anadaiwa kukimbia muda mfupi baada ya kutokea ajali hiyo.

Abiria hao ambao kwa sasa ni majeruhi na wako hospitalini, walisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva Makame aliyekuwa amepokea gari kutoka kwa  dereva mwenzake (jina halijafahamika) na kwamba walitembea masafa mafupi na kupata ajali.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Sokoine, Dk. Jumanne Shija, alithibitisha kupokea  miili ya watu wanne wote wakiume na majeruhi sita.

Alitaja majina ya marehemu kuwa ni Hassan Msata (42) mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, Abdallah Mussa (19) wa Mmumbu, Muhibu Mbaraka (25) mkazi wa Kariakoo mjini Lindi na Samuel Rioba (33) mwenyeji wa Mwanza.

Dk. Shija pia aliwataja majeruhi kuwa ni Robson Molen (26), Sabiini (60) aliyeumia usoni na bega la kushoto, Chapuchapu aliyeumia kichwani, Aziz Mkeka (41), Abdallah Mambo (36), Said Ismail (28), Mwanaidi Ahmed (5), Shufaa Matola (24), Ally  Ngele (41) na mwingine ambaye jina lake halikufahamika mara moja, wote wakazi wa Manispaa ya Lindi.

Alisema katika majeruhi hao, wawili akiwamo dereva wa Kampuni ya Dangote, Ally  Ngele na Abdallah Mambo, wamehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam kutokana na kuumia vibaya maeneo ya kichwani na maeneo mengine ya miili yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) Pudenciana Protas, alipopigiwa simu ili kupata kauli yake, alisema yuko kwenye kikao na kumtaka mwandishi aende kesho ofisini kwake.