Wanufaika HESLB walia kupewa fedha pungufu

26Feb 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanufaika HESLB walia kupewa fedha pungufu

BAADHI ya wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu (TIA) wamelalamika kupewa fedha pungufu na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kuwa hatarini kutoruhusiwa kufanya mitihani ya chuo kwa kushindwa kulipa ada yote.

Mmoja wa wanufaika hao aliiambia Nipashe Dar es Salaam jana kuwa wiki tatu zilizopita, walikamilisha taratibu zote za mikopo, lakini Jumatatu ya juma hili walipewa taarifa ya kupunguzwa kwa fedha za mkopo wa ada ya chuo pasi na kuambiwa kiini cha uamuzi huo.

Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi walibaini kudaiwa fedha nyingi na chuo tofauti na walivyotarajia, yote yakiwa ni matokeo ya fedha za mkopo kupunguzwa.

Mwanafunzi huyo alisema jambo hilo limeleta mkanganyiko kwa kuwa huenda baadhi ya wanafunzi wakashindwa kufanya mitihani kwa kutokukamilisha ada kwa wakati, akibainisha kuwa uongozi wa chuo hauruhusu mwanafunzi kufanya mtihani ikiwa hajalipa ada walau kwa asilimia 70.

"Wiki tatu zijazo tunatarajia kuanza kufanya mitihani na hatutaruhusiwa kufanya kama hujakamilisha ada na tumejaribu kuwasiliana na watu wa vyuo vingine ili tujue kama kuna jambo la namna hii, wanasema hakuna.

"Tulipowasiliana Bodi ya Mikopo, walisema walishatoa taarifa kwa maofisa mikopo ndani ya vyuo, lakini maofisa hao hawakutoa taarifa kwetu sisi wanufaika wa mkopo," alilalamika.

Baada ya kupata taarifa hizo, Nipashe ilimtafuta Ofisa Habari Mwandamizi wa HESLB, Veneranda Malima, ambaye alikiri bodi hiyo kupata malalamiko hayo na kubainisha suala hilo limefanyika kwa vyuo vyote nchini.

Alisema kuna baadhi ya wanafuzi waliongezwa kiwango cha kupokea fedha ya ada tofauti na kile walichotia saini awali na mwaka huu bodi imerudisha kiwango halisi walichotakiwa kupokea, hivyo haijapunguza fedha kama wanavyodai.

"Kuna baadhi viwango vilionekana vimepanda na wengine vimeshuka, lakini kama bodi tuliona tuwarudishie vile viwango stahiki walivyotakiwa kupokea tangu mwanzo," alisema.

Alisema walishafanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa TIA wanaohusika na mikopo ya mwanafunzi na kuwafafanulia kuhusu suala hilo.

Nipashe pia ilimtafuta Ofisa Mikopo wa TIA, Hasani Ayubu, ambaye katika ufafanuzi wake kuhusu suala hilo, alisema idadi ya wanafunzi wanaopatiwa mikopo imeongezeka katika orodha ya kulipiwa ada na serikali na ndicho kiini cha malalamiko hayo.

Wakati baadhi ya wanafunzi wakilalama kupunguzwa kwa fedha za mkopo wa ada, wapo wenzao walioongezwa kiwango cha mkopo huo baada ya awali kupewa fedha kidogo kwa ajili ya ada ya chuo.

Alisema baada ya ongezeko hilo, wale walioongezewa ada mwaka jana, mwaka huu wamepunguziwa na hapo ndipo tatizo lilipoanzia kutokana na wahusika kutoridhishwa na uamuzi huo.

"Jambo hilo limefanyika kwa vyuo vyote nchini, siyo TIA tu. Mwaka huu wale wote wanaosema wamepunguziwa ada, ni zile walizoongezewa mwaka jana.

"Bodi ya Mikopo ilitoa taarifa kwa maofisa wa kila chuo kuhusu suala hilo na tunachokifanya kama viongozi, ni kuwasaidia waweze kuruhusiwa kufanya mitihani kwa wale wasiokamilisha ada," alisema.

Habari Kubwa