Wanufaika wa kaya maskini watengeneza barabara kilomita 7

14Nov 2019
Elizaberth Zaya
Wanging'ombe
Nipashe
Wanufaika wa kaya maskini watengeneza barabara kilomita 7

WANUFAIKA wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), katika kijiji cha Itambo katika Halmashauri ya Wanging'ombe wamegeuka kuwa kivutio baada ya kutengeneza barabara za urefu wa kilomita 7.3 kuelekea katika maeneo ya mashamba ya wakazi wa kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kamati ya wasimamizi wa wanufaika wa Tasaf katika kijiji hicho, David Ngole, alisema mradi huo wa kuchimba barabara uliibuliwa na wanufaika wenyewe baada ya kuona tabu waliyokuwa wakipata wananchi wa kijiji hicho ya kusafirisha mazao yao

Alisema wananchi wengi walikuwa wakilazimika kusafirisha mazao yao kichwani, hivyo kuchukua muda mrefu kufanya kazi hiyo, huku mazao mengine yakiharibikiwa shambani

"Sisi hapa kwetu tunalima sana vitunguu, karoti, hoho, nyanya na viazi. Kwa kipindi kirefu tulikuwa tunahangaika, unakuta mtu amevuna vitunguu vyake, lakini wakati mwingine vinaozea shambani kwa sababu vinasafirishwa kidogo kidogo kichwani kwa sababu hakupitiki na gari,”alisema Ngole.

Aliongeza: "Kwa hiyo Tasaf kupitia miradi ya kuboresha miundombinu inayofadhiliwa na Umoja wa nchi zinaozalisha na kusambaza mafuta duniani ( OPEC) waliwaomba wananchi kuibua miradi ambayo wanaona inatija kwa jamii ndio wakaomba kutengeneza Barabara."

Mariam Mgaya, mnufaika wa Tasaf, alisema walitumia miezi mitano kuchimba barabara hiyo, na kwamba walifanya kazi hiyo kwa ushirikiano na kwa ali kubwa kwa sababu ya taabu waliyokuwa wakipata ni kubwa.

"Na watu walikuwa hawaamini kama tutaweza kutengeneza barabara ikapendeza kwa jembe la mkono, walikuwa wanakuja wanatushangaa, lakini kwa sasa wanatuelewa," alisema Mariam.

Diwali wa Kata ya Mdandu, Annaupendo Gombera, alisema walengwa hao wamekuwa tija kwa wanakijiji kwa kuwa kwa sasa wanasafirisha mazao yao kwa urahisi kwa kutumia magari kutoka shambani

Ofisa Ufuatiliaji wa miradi ya Tasaf Halmashauri ya Wanging'ombe, Edwin Mlowe, alisema mbali na barabara hizo, kuwanufaisha wananchi wa eneo hilo, lakini pia walengwa walipata ajira za muda na kujipatia kipato