Wanunuzi wanaswa utoroshaji wa madini

19Jul 2019
Neema Sawaka
KAHAMA
Nipashe
Wanunuzi wanaswa utoroshaji wa madini

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko, amefanya ukaguzi na kuwakamata wanunuzi wa dhahabu 12 wanaodaiwa kununua madini nje ya masoko yaliyoidhinishwa na serikali wilayani Kahama.

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko.

Imedaiwa kuwa wanunuzi hao walikuwa wanajihusisha na utoroshaji wa madini ya Tanzania kupitia nchi za Kenya na Uganda, wakikwepa kulipa kodi ya serikali.

Vilevile, waziri huyo ameagiza kuwekwa ndani kwa maofisa madini wanaodaiwa kushiriki katika utoroshaji wa madini na kuandaa taarifa za uongo kwa serikali.

Katika ukaguzi huo uliolenga kuwakamata wanunuzi wa madini wanaokwepa kodi uliofanyika katika Halmashauri ya Msalala, wanunuzi 12 walikamatwa wakituhumiwa kununua dhahabu nje ya masoko yaliyoidhinishwa.

Biteko alisema wale wanaoiba madini na kukwepa kulipa kodi ya serikali kwa kununua madini nje ya masoko, wataishia jela na saa ya kunyakuliwa kwao imewadia.

Alidai kuwa kati ya wanunuzi 12 waliokamatwa, imebainika mmoja wao ndani ya wiki mbili, amenunua dhahabu kwa Sh. milioni 300 na mwingine ndani ya wiki tatu amenunua dhahabu ya Sh. milioni 241.

Alisema sekta ya madini ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi endapo kutakuwapo na ushirikiano na kutumia fursa ya kuuza madini kwenye masoko ili kodi stahiki za serikali zilipwe.