Waomba kazi ujenzi wa barabara, wachoka kuwa watazamaji

16May 2019
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Waomba kazi ujenzi wa barabara, wachoka kuwa watazamaji

BAADHI ya wananchi wa Kijiji cha Kitelewasi Wilayani Iringa wamewaomba wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ya barabara kuwapa kazi mbalimbali ili kujipatia kipato badala ya wao kubakia kama watazamaji wa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Akizungumza  mmoja wa wakazi wa kijiji kicho Benedictor  Innocent amesema hayo baada ya kushiriki kujenga makinga maji kwenye barabara ya Lundamatwe- kitelewasi kwenye shughuli ya mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi kutoka wakala wa barabara nchini (Tanroads) na wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) yanayoendelea kwa wiki mbili mjini Iringa chini ya Shirika la kazi duniani (ILO).

Innocent aliomba wananchi kushirikishwa kwenye miradi ili kuepuka kuharibiwa miundombinu na mali zao.

Alisema kuwa awali mradi huo ulipokuja mara ya kwanza hawakushirikishwa wananchi walilalamika kuharibiwa mashamba, vibanda vyao, mabomba ya maji na kuomba pia fursa kama hizo zinapojitokeza  wapewe wakazi wa eneo husika ili wapate fedha kwa ajili ya kujikimu.

Naye Mhandisi wa mazingira kutoka Tarura Dk.Vero Mirambo amesema mafunzo hayo yatakuwa mwanzo mpya wa kujenga barabara zinazodumu kwa muda mrefu hiyo ikiwa ni baada ya kufundishwa namna ya kudhibiti mmomonyoko wa udongo kwenye barabara kwa kupunguza kasi ya maji ya mvua barabarani.

Dk.Mirambo alisema kuwa mawe yakipangwa vizuri vua ikinyesha yatazuia maji yasiende kwa kasi na hivyo mmomonyoko utakuwa umepunguwa.

“Kazi hii ya kutengeneza makinga maji kwa kutumia mawe ambayo yanapatikana kiasilia katika eneo husika itawasaidia pia wanakijiji kupata kazi ya kutwa wakafanya na kuzuia barabara isiharibike na kudumu kwa muda mrefu.”alisema Dk.Mirambo

Kwa upande wake meneja wa Tarura wilaya ya Kilolo Mhandisi Asery Kajange amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza matumizi ya fedha zilizokuwa zikitumika kufanya matengenezo ya barabara mara kwa mara hasa za udongo huku mkufunzi wa mafunzo hayo yanayodhaminiwa na shirika la maendeleo la Ireland Irish Aid Peter Kariuki akisema licha ya mafunzo hayo kupunguza gharama za kujenga barabara mara kwa mara yatasaidia kupunguza migogoro baina ya wakandarasi na wanavijiji.

Habari Kubwa