Waomba kufundishwa matumizi ya umeme wa REA

02Sep 2019
Dotto Lameck
Shinyanga
Nipashe
Waomba kufundishwa matumizi ya umeme wa REA

WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga waliyounganishwa na huduma ya umeme wa mradi wa REA, wameliomba Shirika la Umeme TANESCO Mkoani Shinyanga kutoa elimu juu ya matumizi ya umeme huo ili waweze kujiepusha na hatari inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuwa na elimu juu ya matumizi sahihi.

Ombi hilo wamelitoa jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa SabaSaba. Wananchi hao wamedai kuwa wamekuwa wakiunganishiwa huduma ya umeme bila kupewa maelekezo juu ya namna ya kutumia hali ambayo inawalazimu kuwasha taa usiku na mchana bila kuzima wakihofia kugusa.

Jackson Yohana, mmoja wa wananchi waliohudhuria katika mkutano huo amesema kuwa "Tumekuwa tukiacha taa zinawaka usiku na mchana bila kuzima tukihofia kupata madhara endapo tutagusa sehemu ya kuwashia na kuzimia, lakini mbali na hilo tumekuwa tukiingia gharama, na yote hayo ni kwa sababu hatuna elimu juu ya matumizi sahihi ya umeme," amesema 

Ameongeza kuwa licha ya Serikali ya awamu ya tano kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha inapeleka umeme mpaka Vijijini lakini ni wananchi wachache ambao wameunganishwa na huduma hiyo ambao hawajapewa elimu ya kuitumia umeme huo wa REA.

Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mradi wa REA Shinyanga Vijijini amesema kuwa watatoa elimu kwa wananchi wote ambao tayari wamekwisha unganishwa na umeme huo na ambao bado hawajaunganishwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko ameliagiza Shirika la Umeme TANESCO Mkoa wa Shinyanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya umeme ili kuwaondolea hofu ya matumizi wananchi hao.

Habari Kubwa