Waomba kukutanishwa na Rais Samia 

17Jan 2022
Daniel Sabuni
LOLIONDO
Nipashe
Waomba kukutanishwa na Rais Samia 

WAKAZI wa Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, wamekiomba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwakutanisha na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwasilisha ombi lao la kutaka kuendelea kubakia kwenye ardhi yao yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500.

Uamuzi huo unalenga kupinga kauli ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, ya kuwataka waondoke eneo hilo kwa kuwa liko katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

 Tamko hilo la wananchi, viongozi wa mila wa jamii ya Kimasai (Alaigwanani), madiwani na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Ngorongoro lilisomwa mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Olorieni na Diwani wa Alash, Mathew Siloma.

“Kwa sasa tunaona mtu anayeweza kusikia kilio chetu ni Rais Samia. Mkuu wa Mkoa (Mongela), kwa kujua au kutojua ameuanzisha upya mgogoro uliopo, wakati ulishayapita mamlaka yake ya utawala. Kiujumla amezua taharuki,” alisema.

Alisema kutokana na kauli hiyo wameshaanza mchakato wa kukutana na Rais Samia, kupitia Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ngorongoro.

Alisema kitendo cha Mkuu wa Mkoa, kuanzisha upya mgogoro huo kwa kutembelea eneo hilo na kusema linatengwa, ni kukiuka misingi ya utawala bora, kuingilia mahakama na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi wa Tarafa za Sale na Loliondo.

Siloma, alisema madiwani kutoka kata zinazoathirika, viongozi wa vijiji, viongozi wa mila na wanawake, wanaiomba serikali kupitia kwa Rais Samia, kuchukua hatua za kutambua kilomita za mraba 1,500 kuwa ni ardhi ya vijiji na sio eneo la hifadhi.

 “Tutakutana na Rais Samia ili kumweleza uhalisia wa mgogoro huo wa kutungwa na wahifadhi kwa kuwalinda wawekezaji bila kutambua maslahi ya maisha ya wananchi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum, Tarafa ya Sale, Kijoolu Kakeya, alisema kuwa wanawake wa wilaya hiyo, ndiyo waathirika wakubwa wa migogoro hiyo na  kuomba wamwone Rais Samia awawapiganie.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Ole Senge, akizungumzia mgogoro huo, alisema chama wamepokea malalamiko hayo na watayafikisha kunakohusika yashughulikiwe kwa haki na kupata muafaka.

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mongella, alipokuwa ziarani wilayani humo, alisema serikali imesikia mengi kuhusiana na eneo lenye mgogoro na kusisitiza kuwa serikali haitaonea mtu yeyote.

Habari Kubwa