Waomba uagizaji vilainishi nje upigwe ‘stop’

12Oct 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waomba uagizaji vilainishi nje upigwe ‘stop’

SERIKALI imeombwa kupiga marufuku uagizaji wa mafuta ya kulainisha mitambo kutoka nje ya nchi, ili kuvilinda viwanda vya ndani.

Ombi hilo lilitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Lake Group, Khaled Hassan Mohamed, wakati akizungumza na waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari.

Alikuwa akizungumzia uzinduzi wa kiwanda kipya cha kutengeneza vilainishi vya mitambo cha Lake Lubes Blending Plant kilicho chini ya Lake Group, kilichojengwa Vijibweni Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, anatarajiwa kufungua kiwanda hicho mwanzoni mwa wiki ijayo.

Mohamed alisema viwanda vya ndani vya kutengeneza vilainishi vya mitambo vinauwezo wa kuzalisha vilainishi hivyo kwa ubora wa hali ya juu.

Mohamed alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 45,000 za vilainishi vya aina zote na tayari wameshapata vibali kutoka kwenye taasisi mbalimbali za serikali.

Alisema ingawa vilainishi vingi vinatoka nje ya nchi, lakini baadhi ubora wake haulingani na ule wa vilainishi vinavyozalishwa nchini.

“Wenye magari na mitambo wanalalamikia vilainishi visivyo na ubora sasa sisi tunataka kuja na bidhaa ambayo watumiaji wa vyombo vya moto wataifurahia na tutatoa waranti kama mtu chombo chake kitaharibika kwa kutumia vilainishi vyetu tutamfidia,” alisema Mohamed.

Alisema malighafi za kutengeneza vilainishi hivyo watakuwa wanatoa nchi za Urusi, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu na kwamba Lake Lubes imewekeza Dola za Marekani milioni 4.5.

Alisema kiwanda hicho kinatarajia kuwa na fursa za ajira zipatazo 250 na mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 39, kati ya hao 34 ni wazawa na raia wa kigeni watano na kwamba wanatarajia kuendelea kupunguza raia wa kigeni ili wabaki Watanzania pekee.

Habari Kubwa