Waondolewa hofu madai benki kuuzwa

20Feb 2021
Mary Mosha
Moshi
Nipashe
Waondolewa hofu madai benki kuuzwa

MWENYEKITI wa Bodi ya Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), Dk. Gervas Machimu, amewaondoa hofu wanachama wa ushirika na wateja kuwa benki hiyo haijauzwa kwa CRDB bali wamewekeza ndani ya benki hiyo kimkakati.

Dk. Machimu alisema hayo jana mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, alipofanya ziara katika benki hiyo mjini hapa na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi huku akisisitiza kuwa benki hiyo iko imara. 

"Benki kwa sasa iko imara na wewe umeona mwenyewe katika kipindi cha miezi mitatu tumetoka  hasara  (upotevu) Sh. milioni 345 mpaka Sh. milioni 45. Hii inaonyesha wazi kuwa kazi kubwa imefanyika hasa katika kuboresha misingi ya usalama ndani ya benki na kukuza mtaji," alisema. 

Alisema lengo la kuanzishwa kwa benki hiyo ni kusaidia kuwainua wanaushirika kiuchumi na kudai kuwa tetesi zinazoenea mtaani kuhusu kuuzwa kwa benki hiyo kwa CRDB si za kweli.

Dk. Machimu alisema awali benki hiyo ilikuwa ikipitia  katika matatizo,  lakini kwa sasa imesimama imara na inaendelea kusimamia shughuli za kibenki na kubainisha kuwa mpaka sasa, hisa asilimia 14 zimeshauzwa na kwamba bado kuna fursa ya uwekezaji ndani ya benki hiyo.

“Japo tunaendelea kutoa huduma, tuna mambo tiunayokuomba Katibu Mkuu utusaidie ikiwamo kusukuma mashauri ya watu walioifanyia ubadhirifu benki yetu ambayo yako mahakamani pamoja na kutusaidia kupata Sh. bilioni tatu ambazo zilifanyiwa ubadhirifu,” alisema Dk. Machimu.

Mwenyekiti huyo pia alimwomba Katibu Mkuu kuwasaidia kukamatwa watu walioihujumu benki hiyo ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa akiwamo aliyekuwa ofisa mikopo wa benki.

Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dk. Benson Ndege, aliwataka watumishi wa benki hiyo kuendelea kuwa wabunifu, kuongeza ufanishi kazini na kuwa tayari kupokea matatizo na kuyafanyia kazi. 

Kusaya kwa upande wake aliwataka wafanyakazi wa benki hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kurejesha imani kwa wanaushirika.

Alisema lengo la kuanzishwa kwa benki hiyo ni kuhakikisha inamkomboa mwanaushirika na kuwataka kufanya benki hiyo ifahamike ndani na nje ya nchi kwa kuitangaza.

“Niwatake mhakikishe ndani ya muda mfupi muwe na matawi mengi ndani ya nchi ili wateja wenu popote watakapokuwa wapate huduma. Pia hakikisheni panapokuwa na shughuli za ushirika ndani ya nchi hii, mnaenda kuitangaza benki,” alisema.

Katibu Mkuu pia aliagiza wale wote ambao walikuwa wateja wa benki hiyo na wanadaiwa kuhakikisha wanalipa madeni
haraka na wale wote watakaokaidi, watachukuliwa hatua za kisheria.

Habari Kubwa