Waozesha watoto wa kike kwa pombe

10Dec 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Waozesha watoto wa kike kwa pombe

WANANCHI wa kijiji cha Penzi katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, wamesema ongezeko la mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia vinachangiwa na wazazi kuwaozesha kwa jagi moja la pombe vilabuni.

Hayo waliyabainisha juzi kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, yaliyofanyika katika kijiji cha penzi yaliyodhaminiwa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision chini ya mradi wa Enrich.

Angelina Selemani, mkazi wa kijiji hicho alisema kinababa wamekuwa wakiwaozesha watoto wao wa kike bila kuwajulisha kwa kubadilishana na jagi moja la pombe au ng’ombe wawapo vilabuni.

Alisema kulingana na mila na desturi za Kisukuma, hawaruhusiwi kuhoji, hivyo inabidi mtu akubali mwanawe aolewa japo anasoma na makubaliano yanakuwa yamefanyika kwenye vilabu wakati wanakunywa pombe na wanapokataa wanaambulia vipigo.

Naye Maria Emmanuel alisema: “Wakati mwingine unakuta mtoto anafanya vizuri kwenye masomo yake lakini baba yake anamtaka kufanya vibaya kwenye mitihani yake kwa kisingizio hana fedha ya kumsomesha na unapofuatilia unakuta ameshakula mahari.”

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale, alisema ili kukomesha vitendo hivyo, wameanzisha utaribu wa mtoto wa kike anayefanya vizuri kwenye masomo, mzazi anatakiwa kufunga mkataba na mwalimu mkuu wa shule anayosoma na atakapofanya vibaya, mzazi atawaajibika kisheria.

Ngwale pia alisema hakuna ndoa yoyote itakayofungwa kuanzia ngazi ya kijiji, kata hadi wilaya bila kuwa na cheti cha kuzaliwa ambacho kitaonyesha umri wa anayekwenda kuolewa na akiwa chini ya miaka 18, wazazi wa pande mbili watashtakiwa.

"Kwa sasa mmebuni mbinu mpya ya kuwaozesha watoto wenu. Mnamwozesha binti mwenye umri wa kuolewa mchana na usiku ukifika mnampeleka mtoto wenu kwa mlengwa. Hii mbinu tunaifahamu na tunaifuatilia na lazima tuwabaini na kuwafungulia mashtaka," alisema Ngwale.

Aidha Ofisa Jinsia na Utetezi wa Mradi wa Enrich, Magreth Mambali, alisema wamekuwa wakitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili ikitokea kuwapo vitendo hivyo, watambue wapi wanatakiwa kwenda kupata msaada.

Pia alibainisha kuwa waendesha baskeli na bodabonda wamekuwa chanzo kikubwa cha kusababisha mimba za utotoni kwa watoto wa kike na kutoa wito kwa wadau na serikali kusogeza huduma za kishule hasa elimu ya sekondari karibu na makazi ya watu.

Habari Kubwa