Wapanga kumwona JPM madaktari kukosa ajira

14Feb 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Wapanga kumwona JPM madaktari kukosa ajira

CHAMA cha Madaktari (MAT), kinatarajia kukutana na Rais John Magufuli, wiki ijayo, kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwamo ukosefu wa ajira, udhalilishaji na motisha za watumishi.

Rais wa MAT, Dk. Elisha Osati, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo ambao utashirikisha watumishi zaidi ya 1,000, na kueleza kuwa wanatarajia mkutano huo kufanyika Alhamisi.

“Tumekuwa tukifanya juhudi za kutaka kuonana na kukaa pamoja na Rais Magufuli ili kufanya mazungumzo ya masuala mbalimbali yanayohusu watumishi wa sekta ya afya, ikiwamo pongezi zetu kwa kazi kubwa iliyofanywa na serikali kuboresha huduma,” alisema na kuongeza:

“Leo tunayo furaha kuwataarifu kuwa amekubali ombi letu na yupo tayari kukutana nasi Februari 20, mwaka huu.”

Alisema awali walitarajia kukutana naye Machi 3, mwaka huu, katika Mkutano Mkuu wa MAT, lakini aliomba kurudisha nyuma siku za kukutana.

Alisema mbali na kuelezea mafanikio yanayotokana na juhudi kubwa zilizofanywa na serikali, wanatarajia kueleza kuhusu tatizo la ajira nchini linalotokana na idadi kubwa ya wahitimu wanaozalishwa kutoka vyuoni kila mwaka.

“Kila mwaka wahitimu 1,500 wa taaluma ya udaktari wanaingia mtaani na hakuna ajira, lakini taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa wana upungufu wa madaktari kwa asilimia 51,” alisema Dk. Osati.

Alibainisha zaidi kuwa serikali imejenga hospitali mpya 69 za wilaya na zilizokuwapo ni 70, lakini bado hawajaajiri madaktari.

Alisema ili kuondokana na adha hiyo, wanaishauri serikali kushirikiana na sekta binafsi kuanzisha vituo vya afya nchini ili kusaidia kutoa ajira na huduma bora na za uhakika.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), daktari mmoja anapaswa kutibu wagonjwa 10,000 kwa mwaka, lakini nchini daktari mmoja anatibu wagonjwa 25,000 kwa mwaka, na ukiangalia kweli serikali haina uwezo wa kuajiri wahitimu wote,” alisema Dk. Osati.

Alisema athari nyingine ambayo ilikuwapo, lakini inaendelea kupungua ni wanasiasa kuingia majukumu ya watumishi wa afya kwa ajili ya kujipatia umaarufu.

Kwa mujibu wa Dk. Osati, wanatarajia kuzungumzia suala la motisha na maslahi ya watumishi wa sekta ya afya nchini katika kuendelea kusaidia kuboresha sekta ya afya.

Habari Kubwa