Wapewa mafunzo kujikinga na ebola

11Jan 2019
Gurian Adolf
Katavi
Nipashe
Wapewa mafunzo kujikinga na ebola

MWAKILISHI wa Kanisa Katoliki katika mafunzo maalumu ya kujikinga na ugonjwa wa ebola mkoani Katavi, Padre Monsinyori Kisapa, ameishukuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuyajali madhehebu ya dini kwa kuyashirikisha katika jitihada za kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Akizungumza jana katika mafunzo maalumu ya kukabiliana na ugonjwa huo, alisema Idara ya Afya katika mkoa huo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa viongozi wa dini hawabaki nyuma katika jitihada za kukabiliana na magonjwa mbalimbali kwa kuwapa elimu.

Ofisa Programu Elimu ya Afya kwa umma wa wizara hiyo, Tumaini Haonga, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuelimisha jamii kuchukua tahadhari dhidi ya tishio la mlipuko wa ugonjwa wa ebola na kuwashirikisha wataalamu wa afya, viongozi wa madhehebu ya dini, waganga wa jadi, wazee wa kimila na waandishi wa habari, alisema mafunzo hayo yanatolewa kwakuwa ugonjwa huo tayari umekwisha ripotiwa katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopo hatarini kuambukizwa ebola kutokana na jiografia yake kupakana na nchi ya Kongo na mwingiliano wa kibiashara.

Alisema mpaka sasa Tanzania hakuna mtu yeyote aliyegundulika kuwa na ugonjwa huo, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), wameanza kuweka tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Mkoa wa  Katavi ni miongoni mwa mikoa minane iliyo hatarini kupata ugonjwa huo kutokana na kupakana na nchi ya  Kongo.

Aliitaja mikoa mingine iliyopo hatarini kukumbwa na ugonjwa huo kuwa ni mkoa wa Kigoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Kagera, Dar es Salaam na Mwanza.

Dk. Haonga alisema nchi ambazo zinapakana na maeneo ambayo tayari yamewahi kuripotiwa ugonjwa huo ni lazima zichukue tahadhari kutokana na ugonjwa huo kuongoza kwa vifo na maambukizi kwa kipindi cha kuanzia Agosti, mwaka jana hadi Januari mwaka huu jumla ya watu 370 walifariki dunia nchini Kongo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Omari Sukari, alisema Mkoa wa Katavi  umewekwa tahadhari kuhusu ugonjwa huo na kuweka kituo kimoja cha kupokea wagonjwa wa ebola endapo watatokea.

Aidha, wamehakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana wakati wowote.

Habari Kubwa