Wapinzani wabwagwa kortini, waamua kufungua kesi upya

15Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Wapinzani wabwagwa kortini, waamua kufungua kesi upya

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali kusikiliza kesi ya kupinga Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa na kutakiwa kulipa gharama zote za uendeshaji wa shauri hilo.

Uamuzi huo utolewa jana mahakamani hapo na Jaji Benhaji Masuod, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, ikiwamo ya serikali iliyowasilisha mapingamizi 10, likiwamo la kutaka shauri hilo litupwe kwa sababu mahakama haina mamlaka ya kujadili mambo ya Bunge.

Shauri hilo namba 31 la mwaka 2018, lilifunguliwa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake wawili ambao ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Joran Bashange na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Salum Bimani.

Zitto na wenzake walikuwa wanapinga Kifungu cha 8(3) kinachohusu Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi za Binadamu na Wajibu.

Pia, walikuwa wanapinga maudhui ya muswada huo pamoja na mambo mengine wakidai unapora haki na mamlaka ya vyama vya siasa na kufanya shughuli za kisiasa kuwa jinai.

Shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Masoud, huku upande wa serikali ukiwakilishwa na Mawakili Wakuu wa Serikali Ponziano Lukosi na George Mandepo, pamoja na Wakili wa Serikali Rehema Mtulia na upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Mpale Mpoki, Stephen Mwakibolwa, Daimu Khalifan pamoja Jeremiah Mtobesya.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Masoud alisema anakubaliana na hoja mbili za upande wa serikali kati ya 10 zilizowasilishwa mahakamani hapo ikiwamo ya Zitto na wenzake kuchanganya maombi mawili katika shauri moja.

Jaji Masoud alisema mazingira ya shauri hilo na maombi yaliyowasilishwa, hayakufaa kuunganishwa pamoja, hivyo anakubaliana na upande wa serikali kuwa maombi hayo yanahitaji kuwa tofauti.

Alisema kwa kuzingatia mazingira ya hoja za mapingamizi ya awali ya serikali zilizotolewa, pingamizi namba tatu na sehemu ya pingamizi namba nane, zina mashiko, hivyo shauri halikuletwa mahakamani inavyostahili.

Baada ya kusoma maelezo hayo, Jaji Masoud alisema analitupilia mbali shauri hilo kwa gharama.

Akizungumza nje ya mahakama, Zitto alisema tayari wamewaagiza mawakili wao kufungua upya kesi nyingine.

"Nimewaelekeza mawakili wetu kuwa leo leo (jana), kufungua kesi Mahakama Kuu juu ya kifungu hicho cha 8(3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi za Binadamu na Wajibu," alisema.

Zitto alisema huu ni mwaka kwa wanasiasa kudai demokrasia ya kweli mahakamani na hawatasita wanapoona haki inaminywa ama kuporwa.

Zitto pia alisema anaheshimu uamuzi uliotolewa na Jaji Masoud kuhusiana na kesi yao, lakini tayari wameshachukua hatua ya kufungua tena shauri lingine mahakamani hapo.

Habari Kubwa