Wapotoshaji chanjo ya Corona kushughulikiwa

25Sep 2021
Grace Mwakalinga
Sumbawanga
Nipashe
Wapotoshaji chanjo ya Corona kushughulikiwa

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti, ameliagiza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama, kuwashughulikia wale wanaotoa taarifa za upotoshaji kuhusu umuhimu wa wananchi kupata chanjo ya ugonjwa wa virusi vya corona (Uviko 19).

Aidha amewasisitiza watumishi wote wa Idara ya Afya mkoani humo, kupata chanjo hiyo ili wananchi wawe na imani juu usalama wa chanjo inayotolewa na baadhi yao kuacha kutoa taarifa za upotoshaji.

Mkirikiti ametoa kauli hiyo   baada ya Mkuu wa Wilaya Kalambo, Tano Mwera,  kudai baadhi ya watumishi wake hawamuungi mkono kwenye kampeni ya kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya Uviko 19.

“Serikali  imefanya jitahada za kuwapatia wananchi chanjo kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19 lakini watu wachache wanatoa kauli za kukatisha tamaa, nasema hili halikubaliki “kitaumana” tutawashughulikia,  neno hiyari lisitumike vibaya hatutakubali kuona baadhi yetu wanawaambukiza wenzao kisa hawajapata chanjo kila mwananchi mwenye sifa ya kupata chanjo atachanjwa,” alisema Mkirikiti.

Hata hivyo amewaagiza wakuu wa vyombo vya usalama hususani Jeshi la kujenga Taifa kabla ya vijana wanaopata mafunzo ya kuhitimu wapate chanjo ya Corona sambamba na Jeshi la Polisi kuhakikisha maeneo yote ya biashara kama vile gulio wafanyabiashara wanaoingia na kutoka wanapata chanjo.

Aidha amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Boniface Kasululu,  kufungua vituo vya utoaji chanjo kwenye maeneo mbalimbali ili  kuwapungua gharama wananchi kufuata huduma hiyo kwenye vituo vya afya vilivyokuwa vimepangwa awali.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Boniface Kasululu amesema Mkoa ulipokea jumla ya chanjo 20000 za Uviko na kwamba hadi sasa ni watu 3100 tu sawa na asilimia 15  ndio wamechanjwa.

Amebainisha kuwa  Wilaya ya Nkasi jumla ya chanjo 4800 Filitolewa na kwamba watu 542 ndio wamepata chanjo hiyo, Kalambo jumla ya chanjo 2400 zilitolewa na wananchi wameopata ni watu 233.

Amesema idadi ya waliochanjwa ni ndogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo imani potofu  kwamba chanjo hizo zinaathari kiafya jambo ambalo sio kweli.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Tano Mwera amesema imani potofu kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo kumechangia zoezi la chanjo kutofanikiwa kama ilivyokusudiwa huku akiwalalamikia watendaji wa kata, vijiji na wenyeviti kutomuunga mkono katika jitahada za kuhamasisha utaoji wa chanjo ya Uviko 19.

Kwa upande wake Chifu Charles Katata kutoka Himaya ya Nkasi Milanzi ambaye pia Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu mkoani Rukwa amesema yeye ni miongoni mwa watu waliopata chanjo siku za mwanzo na kwamba hakuna madhara yeyote aliyoyapata.

Amesema kwa imani zao,  walijiridhisha na ubora na usalama wa chanjo hizo hivyo  aliwahamasisha na wengine kuchanjwa ili kuimarisha kinga za mwili katika kupambana na ugonjwa huo.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT), Dayosisi ya Ziwa Tanganyika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa,  Ambele Mwaipopo amesema  baadhi ya waumini waliingiwa na hofu juu ya chanjo hiyo baada ya kudanganywa kuwa ni alama za 666  inayozungumwa kwenye biblia jambo ambalo alikanusha.

Amesema kwa umuhimu wa chanjo hiyo yeye ni miongoni mwa waliopata na kwamba amekuwa na utaratibu wa kuhamasisha waumini wake eote kuchanjwa.

Ofisa Programu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Zainabu Nyamungumi amesema hali ya utaoji chanjo wilayani humo hairidhishi aliwasisitiza viongozi hususani watumishi wa idara ya Afya,  kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi ili kumaliza dozi zilizobakia.

Habari Kubwa