Warioba aonya udini na ukabila

13Oct 2021
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Warioba aonya udini na ukabila

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amewataka viongozi na Watanzania kuwakemea wanaoleta ukabila, udini, ukanda na vyama, akisisitiza ameanza kushuhudia vitendo hivyo nchini.

Jaji Warioba aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam katika kongamano la kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Kigamboni.

Akizungumza katika kongamano hilo, Jaji Warioba alikumbusha kuwa juzi Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia kuhusu suala hilo wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni na kuonya vitendo vya kuendekeza ukabila nchini.

Alisema mambo hayo ndiyo msingi wa kujenga umoja, mshikamano na amani, ambayo anaona yanaanza kuchezewa.

"Ni ukweli kwa sasa unaweza kukuta ukabila unaanza kuzungumzwa sana, udini unaanza kuzungumzwa sana, ukanda unaanza kuzungumzwa sana, ujana unaanza kuzungumzwa sana, ile misingi ambayo ilijenga umoja na amani katika nchi tunaanza kuingiliwa," Jaji Warioba alionya.

Alikumbusha kuwa Machi 1995, Mwalimu Nyerere alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, alizungumzia nyufa na kati yake alizitaja kuwa ni zile ambazo zinavunja umoja.

“Ninadhani tuna jukumu Watanzania, viongozi na wananchi wa kawaida, tukemee watu wote ambao wanataka kuleta mambo ya ukabila, mambo ya udini, mambo ya ukanda na mambo ya vyama. Watanzania tuwe kitu kimoja, tujivunie misingi yetu iliyojengwa tangu awali.

“Amani ilijengwa wakati Mwalimu Nyerere anapigania uhuru, alikuwa na nia ya dhati ya kulijenga taifa lenye umoja na amani. Siku hizi tunazungumza (amani) kama ilikuwa kazi rahisi.

“Aliposema tutumie Kiswahili, siku hizi mnaona jambo la kawaida, wakati ule ilikuwa siyo kawaida, kulikuwa na makabila ambayo yalitafsiri mpaka vitabu vitakatifu katika lugha yao. Kama kuna kitu kimetuunganisha ni lugha yetu, ninadhani tufike mahali elimu yetu yote iwe katika lugha ya Kiswahili," alisema.

Alisema Mwalimu hakuwa na ukabila, rangi wala dini na watu wake wa karibu, akiwamo Rashid Kawawa (aliyekuwa Waziri Mkuu) alikuwa kabila lingine na dini nyingine lakini aliishi naye kwa kuamini ni Mtanzania mwenzake.

"Aliishi bila ubaguzi, hata maadui zake wanakubali Mwalimu alikuwa mtu wa kawaida, alitumikia nchi hii, hakuiibia, Mwalimu aliishi kama mtu wa kawaida, hakupenda sifa, alipochaguliwa kuwa Rais walimwita mtukufu, alikataa, akasema binadamu hawezi kuwa mtukufu, ni Mungu peke yake, ndiyo chanzo cha kuitwa Mwalimu," alisema.

Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Shadrack Mwakalila, alisema kongamano la mwaka huu limebebwa na kaulimbiu ya 'Maono ya Mwalimu Nyerere katika uongozi, maadili, umoja, na amani kwa maendeleo ya jamii' na wamewaita waliowahi kufanya kazi na Baba wa Taifa ili kuwakumbusha Watanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Stephen Wasira, alisema hafahamu kiongozi mwingine wa kulinganishwa na Mwalimu Nyerere kwa kuwa amekuwa Rais kwa miaka 24 na amestaafu bila ya kuwa na fedha ndani na nje ya nchi na hajawaibia Watanzania.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, alisema Mwalimu alijenga umoja wa viongozi, akifafanua: "Mwalimu aliamini umoja unajengwa kwa vikao, alikuwa muumini wa uamuzi wa kikao, alipokuwa na wazo alilileta katika kikao na lilijadiliwa kwa pamoja na kupata uamuzi."

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema Mwalimu alikuwa mtu mwenye utu, akifafanua: "Ukiwa kiongozi hakikisha vitu vyote ni vya wote, siyo vyako. Mwalimu hakuvifanya vyake, aliviacha viwe vyetu, maadili siyo kusema tusiibe halafu wewe unaiba, unaweka utaratibu wa kuutumikia kwa faida ya wote, siyo ya mtu binafsi."

Habari Kubwa