Wasakwa madai kufukua kaburi, kukata kichwa cha marehemu

29Jul 2021
Gurian Adolf
Sumbawanga
Nipashe
Wasakwa madai kufukua kaburi, kukata kichwa cha marehemu

JESHIl la Polisi mkoani Rukwa linawasaka watu wasiojulikana wanaodaiwa kufukua kaburi kisha kukata kichwa cha marehemu na kwenda kukitelekeza kwenye kichanja cha kuanikia vyombo kwenye nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Kirando wilayani Nkasi.

Regina Samiel mkazi wa familia ambayo watu hao walitelekeza kichwa hicho, alisema Julai 27, aliamka majira ya alfajiri ili atoke nje kwenda kujisaidia.

Alisema alipofungua mlango wa nyumba yao alihisi harufu kali iliyomfanya ashindwe kuvumilia kutoka nje, hivyo kufunga mlango na baadaye kumuasha mama yake na kumsimulia hali aliyoikuta nje.

Alisema baada ya kusubiri kidogo kupambazuke, ndipo alipotoka nje akiwa na mama yake na wakakuta kwenye kichanja cha kuanikia vyombo kilichopo nje mbele ya nyumba yao kuna sufuria kubwa kiasi likiwa limewekwa juu ya kichanja hicho, huku nzi wakiwa wamelizingira sufuria hilo.

Regina alisema baada ya kulisogelea sufuria hilo walikuta kuna kichwa cha mtu, kikiwa kimeharibika na kutoa harufu kali.

Waliamua kutoa taarifa kwa serikali ya kijiji ambayo iliwasiliana na polisi kituo cha Kiranda, ambao walifika na kufanya uchunguzi, na kwamba walipokwenda makaburuni walibaini watu wasiofahamika walifukua kaburi na kisha kukata kichwa cha marehemu na kwenda kukitelekeza kwenye nyumba hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, William Mwampaghale, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu, huku uchunguzi ukiendelea.