Wasichana 500 chini ya miaka 18 wakutwa kwenye ndoa 

13Jan 2018
Renatha Msungu
Nipashe
Wasichana 500 chini ya miaka 18 wakutwa kwenye ndoa 

WASICHANA 500 walio chini ya umri wa miaka 18 wamekutwa katika ndoa za utotoni, huku wengine wakiwa hawajui vizuri kusoma na kuandika.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilipata idadi hiyo katika kata za Segela, Kongwa na Bahi.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya walimu na maofisa elimu wa wilaya ya Bahi na Kongwa, Mkufunzi Mkazi wa Elimu ya Watu Wazima, Habibu Muyula, alisema hali hiyo inatia hofu kutokana na vijana wa rika hilo kuwa wadogo.

Hata hivyo, alisema katika mradi huo ambao unaendeshwa kwa awamu, utatumika kuzikomboa kata ambazo zina watu wa aina hiyo ili kuhakikisha wanajitambua.

Alisema moja ya elimu watakayoitoa ni pamoja na kujitambua, kujua haki zao, kujua mazingira, na uraia wao katika sehemu ambayo wanatakiwa wawe.

Alisema lengo lao ni kuona kila msichana anapata haki yake katika mazingira stahiki, na kupitia mradi huo wa kupinga ukatili wa ndoa za utotoni, unaosimamiwa na taasisi hiyo, Sido na Kiwohede, wanaamini watafanikiwa.Alisema idadi hiyo inatakiwa kupunguza ikiwezekana kutokomezwa katika kata hizo ambazo zitaanza.

Gosbert Damaza, aliyemwakilisha Ofisa Elimu wa mkoa, alisema anaipongeza taasisi hiyo  na kuitaka kuongeza bidii katika suala hilo.

Alisema ni jambo jema na anaamini kupitia mradi huo wa kupinga ndoa za utotoni watafanikiwa kuwainua wasichana wengi ambao wameathirika na ndoa hizo.

Alisema anaungana nao katika kuendelza gurudumu la kupambana na ndoa za utotoni ambazo ni tatizo sugu.

Alisema watakuwa pamoja kushirikiana, kuhakikisha wanafanikiwa kuwakomboa watoto wa kike katika ndoa za utotoni.

Alisema suala hilo linapaswa kupigiwa kelele ili wazazi waache kuoza watoto  badala yake wawapeleke shuleni kwa ajili ya kutimiza ndoto zao.

Alisema hakuna sababu ya kukatisha ndoto ya mtoto wa kike kwa kuwa anahitaji kusoma kama alivyo mtoto wa kiume.