Wasichana wang’ara tuzo za mwanafunzi bora ARU

04Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wasichana wang’ara tuzo za mwanafunzi bora ARU

KWA mwaka wa tatu mfululizo wanafunzi wa kike wamewapiku wavulana na kuongoza kwa kutwaa tuzo nyingi za wanafunzi bora katika Chuo Kikuu Ardhi (ARU).

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Profesa Evaristo Liwa, akimkabidhi tuzo msichana aliyefanya vizuri zaidi kwenye masomo ya mwaka 2020/21 kwa wasichana, Grace Mhina wakati wa sherehe za kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri zilizofanyika chuoni hapo siku ya Ijumaa. Kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia taaluma, Profesa Gabriel Kasenga.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Gabriel Kassenga wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo yao kabla ya mahafali yanayofanyika siku ya Jumamosi.

Jumla ya tuzo 135 zilitolewa kwenye hafla hiyo na kati ya tuzo hizo, 74 ambazo ni wastani wa asilimia 54.8 ya zawadi zote zimechukuliwa na wasichana na 61 ambazo ni asilimia 45.2 zimechukuliwa na wavulana.

Alisema ingawa idadi ya wasichana chuoni hapo ni asilimia 40 lakini wamekuwa wakifanya vizuri na kutwaa tuzo hali ambayo inadhihirisha kwamba wasichana wanauwezo wa kufanya vyema kwenye masomo ya sayansi kinyume na fikra za baadhi ya watu.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Profesa Evaristo Liwa, akimkabidhi tuzo msichana aliyefanya vizuri zaidi kwenye masomo ya mwaka 2020/21 kwa wasichana, Grace Mhina wakati wa sherehe za kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri zilizofanyika chuoni hapo siku ya Ijumaa. Kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia taaluma, Profesa Gabriel Kasenga.

“Katika ushindi wa jumla wanafunzi wawili wamefungana kwa alama ambao ni msichana na mvulana hivyo utaona kwamba wasichana wamepata tuzo nyingi kuliko wavulana ingawa kwa idadi wasichana ni wachache hapa chuoni kulinganisha na idadi ya wavulana,” alisema

Aliwapongeza wanafunzi wote waliopokea tuzo hizo na kuwasihi waendelee kusoma kwa bidii ili waje kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wenzao na jamiikwa ujumla.

“Napenda kuwapongeza wanafunzi wahitimu kwa kujinyakulia tuzo mbalimbali na wengine wamekuwa wakitwaa tuzo kama hizi  kwa miaka yote wakiwa chuoni hapa hii inamaanisha kwamba kwenye juhudi ya kweli mafanikio hupatikana,” alisema

 Baadhi ya washiriki wa sherehe za kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri zilizofanyika chuoni hapo siku ya Ijumaa.

Alisema sherehe hizo ambazo hufanyika kila mwaka ni muhimu kwani hutoa hamasa kwa wanafunzi wa chuo hicho ili waendelee kuweka juhudi kwenye masomo na hatimaye waweze kupata ufaulu wa juu.

Profesa Kassenga alisema sherehe hizo zimekuwa zikiwezeshwa na wadau mbalimbali kwa kujitolea ufadhili wa hali na mali kwa wanafunzi waliofuzu kupata tuzo hizo na aliwaomba wasichoke kuwasaidia kufadhili tuzo hizo.

Alisema zawadi mbalimbali zinazotolewa na wafadhili hao zimekuwa zikiwasaidia wanafunzi hao kuongeza mitaji na utendaji kazi mara wanapomaliza masomo yao.

Viongozi wa meza kuu wakiwa wamesimama kwaajili ya kuanza zoezi la kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kwenye hafla ya kuwatunuku wanafunzi bora wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), ambapo jumla ya tuzo 135 zilitolewa na kati ya hizo 74 kuchukuliwa na wasichna na 61 wavulana.

Habari Kubwa