Wasimamizi uchaguzi wakumbushwa wajibu

17Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wasimamizi uchaguzi wakumbushwa wajibu

WASIMAMIZI wasaidizi wa uchaguzi wamekumbushwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kusimamia uchaguzi, ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa mwezi ujao.

Kaimu Mkuu wa sehemu ya Uchaguzi Kanda ya Pwani kutoka NEC, Stephen Elisante.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo iliyowakumbusha wasimamizi hao wajibu wao wa kukumbuka hayo kwa ajili ya uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Februari 17, 2018.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkuu wa sehemu ya Uchaguzi Kanda ya Pwani kutoka NEC, Stephen Elisante, alipokuwa akifungua mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo la Kinondoni na Kata za jimbo hilo la jiji la Dar es Salaam.

Alisema wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kutambua kuwa uchaguzi ni mchakato unaohusisha taratibu mbalimbali kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, taratibu, maelekezo na miongozo iliyotolewa kisheria.

“Hivyo mnapaswa kuzisoma sheria hizo ili kuweze kutekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria, tufanye maamuzi yetu kwa kujitambua, kujiamini na kutoogopa na kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza,” alisema Elisante.

Aliwakumbusha wasimamizi hao kuwa Tume imekuwa ikisisitiza kwamba sheria za uchaguzi hazikuacha ombwe katika kueleza jinsi gani masuala ya uchaguzi yanatakiwa yatatuliwe. 

Habari Kubwa