Wasimamizi wa uchaguzi mkuu watakiwa kuhakiki vituo mapema

03Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
Wasimamizi wa uchaguzi mkuu watakiwa kuhakiki vituo mapema

Wasimamizi wa uchaguzi nchini wametakiwa kuhakiki vituo na maeneo yao wanayoyasimamia mapema na kubaini changamoto zilizopo mapema na kuzitatua kabla ya siku ya uchaguzi unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba tarehe 28 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akizungumza na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ofisini kwake leo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akizungumza na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambaye yupo Jijini Mwanza kwa ajili ya mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi wa Mkoa wa Mwanza na Mara alipofika ofisini kwake Jijini Mwanza.

Mongella  alisema Ofisi yake itashirikiana na wasimamizi wa uchaguzi mkoani Mwanza na kukagua maeneo ya vituo vya kupigia kura ili kuona changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kufika huko na kuyatatua kabla ya siku ya kupiga Kura.

Ameongeza kuwa, changamoto kubwa iliyopo katika maeneo ya visiwa vilivyopo mkoani Mwanza na kutolea mfano Kisiwa cha Ukerewe ambapo baadhi ya maeneo ni lazima kutumia boti na mitumbwi ndipo ufike, hivyo ni lazima ijulikane mapema hali ya usafiri utakao tumika ili kuhakikisha vifaa vinafika salama na kurudisha ili kufanikisha uchaguzi kwa salama. 

"Elimu itolewe ya watu kujitokeza kupiga kura, tuondoe dhana ambayo imejengeka kwa baadhi ya wapiga kura kuwa fulani ameshashinda na kwamba kila kitu kipo sawa na kuacha kwenda kupiga kura, ni vema wananchi wakaelemishwa umuhimu wa kujitokeza kupiga kura"anaeleza Mongella.

Naye Jaji Mstaafu Mihayo amesema kuwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao tume imeshaanza kusambaza vifaa vya uchaguzi mapema ili kuhakikisha kwamba tatizo la ukosefu /upungufu wa vifaa katika vituo vya kupigia kura halijitokezi kabisa. 

Pia akizungumzia suala la  Elimu ya Mpiga Kura Jaji Mihayo amesema tume italifanyia kazi na kwamba kwa bahati mbaya katika nchi yetu upigaji kura ni suala la hiyari siyo lazima kama ilivyo katika baadhi ya nchi na kwamba mshindi anapatikana kutokana na  wingi wa kura alizopata. 

Pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali kwa asasi za kiraia 245 nchi nzima kwa ajili ya kutoa elimu ya Mpiga Kura juu ya Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu ambapo wananchi watapiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.

Habari Kubwa