Wasimamizi watakiwa kuheshimu sheria

08Aug 2020
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe
Wasimamizi watakiwa kuheshimu sheria

WASIMAMIZI wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Mtwara, wametakiwa kuheshimu sheria za uchaguzi na kanuni zake zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Pia wamehimizwa kushirikisha vyama vya siasa na wadau wengine katika masuala ambayo wadau hao wanastahili kushirikishwa ili kuepuka hali ya kutoelewana itakayotokea katika uchaguzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Changwa Mkwazu, alisema hayo jana alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi hao yaliyofanyika katika ukumbi wa zamani wa halmashuri mjini hapa.

Alisema wasaidizi hao wa uchaguzi 68 ngazi ya kata wanapaswa kutambua kuwa wameaminiwa na kuthaminiwa na NEC, hivyo kupewa jukumu la kusimamia uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28. Kutokana na hali hiyo, aliwataka wafuate kikamilifu sheria za uchaguzi.

Mkwazu alisema jukumu kubwa ambalo wanatakiwa kulifuata ni pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Mnatakiwa kutambua kuwa mmeaminiwa na kuteuliwa kwa sababu mnao uwezo wa kufanya kazi hii. Mambo muhimu mnayotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kujitambua na kwamba mnapaswa kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake,” alisema Mkwazu.

Alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuhisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwa kuwa ndizo msingi wa uchaguzi kuwa wa amani na utulivu.

Mkwazu alisema iwapo wasimamizi hao watafanya kazi kwa ufanisi, wataondoa malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwapa uwelewa wa kutosha ili katika kutekeleza mchakato huo, wawe na elimu nzuri ya kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi.

Habari Kubwa