Wasomi, wanaharakati wafurahia bajeti

11Jun 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Wasomi, wanaharakati wafurahia bajeti

WASOMI na wanaharakati wamefurahia bajeti kwa kuiita yenye ubunifu, inayogusa haki zote za kiuchumi na kutoa suluhisho kwa hati chafu za halmashauri nyingi nchini.

Wakizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema bajeti imepulizwa zaidi na imekuwa na ubunifu tofauti na bajeti nyingine zilizopita.

Alitoa mfano wa posho kwa watendaji kata na maofisa tarafa ambao waliishi kwa hisani ya Wakurugenzi wa Halmashauri wakati wana jukumu la kukusanya mapato na ndiyo maana Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliibua upotevu wa fedha.

“Hawa watendaji kata na maofisa tarafa hawakuwa na nauli za kwenda na kurudi vituo vyao vya kazi, ila sasa watalipwa posho kisheria, sasa tunaona usimamizi utaongezeka, hati chafu zitapoungua,” alisema.

Henga alisema pia kuna ubunifu kwenye malipo ya wastaafu kutoka hati fungani za serikali ambazo zitalipa kwa ahadi jambo ambalo litasaidia kufufua mifuko ya hifadhi ya jamii.

Eneo jingine ni malipo ya wazabuni ambayo CAG alisema changamoto kubwa zabuni anatoza bei ya juu kwa kuwa wanachelewa kulipwa, lakini kwa fedha kutengwa maana yake serikali itaokoa fedha nyingi na kulipa kwa wakati.

Naye, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Razaki Lokina, alisema bajeti imegusa maisha ya wananchi wa kawaida.

“Ukiingalia kwa haraka bajeti hii imegusa wananchi wa kawaida kabisa kwenye afya, miundombinu, maji na afya jambo ambalo linagusa wananchi wengi,” alisema.

Alisema licha ya kodi kuongezwa kwenye mafuta kwa ajili ya kuwezesha matengenezo ya barabara na gharama za usafiri kupanda, lakini itakuwa ni kwa manufaa ya wananchi.

“Ni muhimu kukusanya mapato ili matumizi yanayotakiwa yafanyike, ni muhimu mchakamchaka wa kuzipata hizo fedha ukaanza ili kilicholengwa kunufaisha wananchi wa kawaida kitimie,” alisema Profesa Lokina.

Habari Kubwa