Wastaafu kukoleza moto kampeni CCM awamu ya 3

28Sep 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Wastaafu kukoleza moto kampeni CCM awamu ya 3

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuelekea siku 30 za mwisho za kampeni watakazozianza leo, kitaongeza ‘injini’ mpya kwa kuwatumia mawaziri wakuu wastaafu, marais wastaafu na makada waandamizi, watakaofanya mashambulizi mapya kila kona ya nchi.

Kimesema mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli atazitumia siku hizo kutoa maelezo yaliyosheheni takwimu sahihi, maono yake kwa Watanzania pamoja na kueleza yaliyomo kwenye ilani ya chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole, aliyasema hayo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu awamu ya tatu ya kampeni za urais wa chama hicho, zitakazoanza leo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwamo, Iringa na Mbeya.

“Zitakuwa ni siku 30 kuu, Dk. John Magufuli ataendelea kesho (leo) na mzunguko wake wa kampeni akitokea mkoani Dodoma kuelekea Iringa na njiani atahutubia na kusalimia wananchi, pamoja na kuomba kura zake, madiwani na wabunge,” alisema Polepole na kuongeza:

“Akifika Iringa atafanya mkutano mkubwa katika Uwanja wa Samora, kesho yake ataelekea mkoani Mbeya akipitia mkoani Njombe, Makambako nako atafanya mikutano njiani, Septemba 30 atawasili mkoani Mbeya na kufanya mkutano mkubwa,” alisema Polepole.

Aliongeza kuwa Dk. Magufuli atazitumia siku hizo kutoa takwimu sahihi kwa kueleza nchi ilipotoka, ilipo na inapokwenda kwa kutumia ilani ya CCM.

Aidha, Polepole alieleza kuwa Dk. Magufuli hatatumia majukwaa kujibizana na wagombea wengine wa vyama vya siasa, bali atajikita katika Ilani kwa kuelezea mustakabari wa Taifa kwa miaka ijayo.

“Watanzania wajiandae kupokea ujumbe wa amani, siku zilizobaki tutaongeza injini mpya katika kampeni, mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC, Kassim Majaliwa, mawaziri wakuu wastaafu na makada mbalimbali watatumika kushambulia kila kona, tunakwenda kuwamaliza wapinzani,” alisema Polepole.

Alisema zitakuwa ni siku 30 za kueleza namna ya kuibadilisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Pwani, Kilimanjaro, Dodoma na Tanzania yote, kwamba zitakuwa ni siku za maangamizi kwa upinzani.

AKANUSHA UZUSHI

Aidha, Polepole alikanusha taarifa zilizotolewa na mmoja wa wagombea urais wa upinzani kwamba Rais John Magufuli amewaita Wakurugenzi wa Halmashauri mjini Dodoma na kufanya nao vikao vya siri.

Polepole alisema: “Ni taarifa za uzushi, uongo zenye kuwafitinisha Watanzania, tunaiomba TAMISEMI watolee ufafanuzi.

ALAANI MAUAJI

Wakati huohuo, Polepole alilaani kifo cha Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Vyuo Vikuu mkoani Iringa, Emmanuel Mlelwa, anayedaiwa kuuawa na watu wasiojulikana.

Polepole alisema CCM wana taarifa za waliohusika na kifo cha Mlelwa, kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuwakamata wote waliohusika na kifo hicho.

“Mwili wake ulikutwa eneo la Kibena Bwawani ukiwa umeumizwa na amefariki… nitoe rai kwa Jeshi la Polisi lihakikishe ukweli unafahamika na hatua kali zinachukuliwa kwa wote waliohusika na tukio hilo, kijana huyu alikuwa na ndoto zake,” alisema Polepole.

Habari Kubwa