Wataalam 48 wa afya wapata mafunzo ya dawa za usingizi, ganzi

11Jun 2021
Mary Geofrey
DAR ES SAALAAM
Nipashe
Wataalam 48 wa afya wapata mafunzo ya dawa za usingizi, ganzi

WATAALAM 48 wa afya kutoka vituo mbalimbali vya afya nchini, wamepata mafunzo ya dawa za usingizi na ganzi, kwa lengo la kuongeza wataalam hao katika maeneo ambako wanatoa huduma za upasuaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akikabidhi cheti, Craft Ditick Ng’itu kutoka Mkoa wa Lindi, Halmashauri ya Mtama katika kituo cha Afya cha Nyanganala.

Mafunzo hayo yametolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa muongozo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru, akizungumza leo jijini Dar es Salaam, wakati akiwatunuku vyeti wahitimu hao, amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa muda wa kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja.

“Mtakumbuka kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya nchini kuanzia ngazi ya taifa hadi kwenye Zahanati.

“Kutokana na mageuzi hayo kumekuwa na uhaba wa watalaamu wa dawa za usingizi na ganzi hivyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI zilikuja na mpango wa kusomesha watalaamu hao ngazi ya cheti watakaosaidia kutoa huduma hiyo kwenye  vituo vya afya na hospitali za wilaya zenye uhaba huo” amesema, Prof. Museru.

Amesema tangu wameanza mafunzo hayo miaka sita iliyopita, wamefundisha zaidi ya wataalamu 400 kwa Dar es Salaam na mikoa jirani, kati yao watalaamu 150 kutoka halmashauri mbalimbali nchini.

“Nafurahi pia katika kundi hili la wahitimu 48 baadhi yao wametokea Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya kutoka Mafia, Lindi, Mtama, Rufiji, Kasulu, Kibondo na maeneo mengine na zoezi hili ni endelevu”, amesema Prof. Museru.

Amewahimiza kufanya kazi kwa weledi na kujituma watakaporudi vituo vyao vya kazi ili kuonyesha mabadiliko ya uwapo wao baada ya mafunzo.

Prof. Museru amesema MNH imeboresha huduma zake kwa viwango vya ubingwa na ubobezi hivyo alizataka hospitali zote nchini ngazi ya kanda, mkoa, wilaya na vituo vya afya kuendelea kuitumia ili kufundisha watalaamu wake katika maeneo mengi ambayo wana changamoto ama ya watalaamu.

Habari Kubwa