Wataalamu wa afya na mazingira watakiwa kujisajili

23Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Wataalamu wa afya na mazingira watakiwa kujisajili

Wataalamu wa afya na mazingira nchini wametakiwa kujitokeza kujisajili na kuhuisha leseni zao ili waweze kutambulika na kupata nafasi ya kufanya kazi kwa weledi na bila usumbufu.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Eliud Eliakim wakati alipomuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Mazingira la awamu ya nne kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma. 

Dk. Eliakim amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamefanikiwa kuhuisha mwongozo wa maadili na nidhamu kwa watumishi wa umma ambapo kila baraza limetakiwa kufuata mwongozo huo ili lisimamie maadili na nidhamu ya taaluma husika.

Baraza la Afya ya Mazingira limetakiwa kuhakikisha wataalam wote wa afya ya mazingira wakiwemo maafisa afya nchini wanajitokeza kujisajili na kuhuisha leseni zao ili waweze kusimamia vyema mazingira kwa kutoa miongozo na kufanya usafi ili kuweza kuepuka magonjwa ya milipuko yanayoweza kujitokeza.

Aidha, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali amelitaka baraza hilo kupitia upya sheria kwa kuangalia maeneo muhimu kwa ajili ya kufanya maboresho na pia kumshauri waziri ili kutengeneza kanuni chini ya sheria ya usajili sura 428.

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa