Wataalamu wa uvuvi kupata ajira kimataifa

22May 2020
Gwamaka Alipipi
DODOMA
Nipashe
Wataalamu wa uvuvi kupata ajira kimataifa

WATAALAMU wa vyombo vya uvuvi nchini wataanza kuajiriwa kitaifa na kimataifa, baada ya Bunge kuridhia mkataba wa kimataifa wa viwango vya mafunzo na utoaji vyeti kwa wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi wa mwaka 1995.

Akisoma mkataba huo bungeni jijini hapa jana, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema kuridhiwa kwa mkataba huo kutaleta manufaa tisa kwa taifa.

Dk. Kalemani alisema kwanza utatoa fursa za ajira za ndani na za kimataifa kwa wataalamu wa vyombo vya uvuvi.

Alisema pia kutahakikisha kuwapo kwa ukaguzi wa waangalizi wenye weledi ambao kuwapo kwao kutahakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

“Kutaimarisha vyuo vya ndani vya mafunzo ya uvuvi na kutambulika kimataifa, kuwapo kwa viwango bora vya ufundishaji wa wanafunzi katika vyuo vya uvuvi nchini,” alisema Waziri Kalemani.

Alisema kuidhinishwa kwa mkataba huo kutaimarisha usalama wa wafanyakazi katika vyombo vya uvuvi na hivyo kupunguza ajali.

“Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1994, kazi ya uvuvi ilionekana kuwa ni kati ya kazi hatari duniani kwa kusababisha wastani wa wavuvi 24,000 kupoteza maisha kila mwaka. Idadi hii ni zaidi ya mara 10 ya vifo vinavyotokea katika meli za biashara,” alisema Waziri Kalemani.

Alisema mkataba huo pia utawezesha kuimarika kwa ulinzi, usalama na uhifadhi wa mazingira ya bahari pamoja na kuimarisha kwa upatikanaji wa takwimu na taarifa mbalimbali katika sekta ya uvuvi.

Alisema manufaa ya kupitishwa kwa azimio hilo ni pamoja na kuwezesha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi kutoa mafunzo na vyeti vinavyotambulika kimataifa katika uvuvi wa vyombo vya bahari kuu.

Waziri Kalemani alisema baadhi ya madhara yanayoweza kutokea iwapo mkataba huo hautaridhiwa ni pamoja na Watanzania kutoajirika katika nafasi za kimataifa eneo la uvuvi wa bahari kuu, kinyume na wale wanaofanya kazi katika meli za biashara.

Alisema pia Tanzania itakosa nguvu za ukaguzi na uangalizi wenye weledi kwa meli za kimataifa zinazofanya kazi katika bahari kuu kwa ajili ya kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Alisema kutasababisha kukosekana kwa usimamizi wa ulinzi, usalama na uchafuzi wa mazingira ya bahari, Tanzania kutoonekana kuwa eneo salama la kuvua samaki kwa kutofikia viwango vya kimataifa.

Alisema Tanzania itakosa mapato kutokana na kukosekana kwa ajira za Watanzania katika soko la kimataifa.

Akisoma ushauri wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Mchafu, alisema ni muhimu kwa serikali kuzingatia mikataba ambayo ni mizuri na yenye faida kwa nchi na kuiwasilisha bungeni ili kuridhiwa mapema na kuanza kunufaika badala ya kusubiri athari zitokee.

Alisema ni muhimu serikali iharakishe kuandaa sera ya bahari kwa kuwa ni muhimu hasa kama nchi inataka kuwekeza na kunufaika na uchumi unaotokana na bahari.

Vilevile alishauri Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kuimarishwa na kuboreshwa kwa kuhakikisha linakuwa na vitendea kazi bora na vyenye kukidhi viwango vya Taifa na kimataifa kwenye kufanya ukaguzi.

Habari Kubwa