Wataalamu watoa angalizo upotoshaji chanjo corona

05Dec 2021
Shaban Njia
Kahama
Nipashe Jumapili
Wataalamu watoa angalizo upotoshaji chanjo corona

​​​​​​​WATAALAMU wa afya wametoa angalizo kwa wananchi dhidi ya upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kuhusu usalama wa chanjo za ugonjwa wa UVIKO-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Wamesema kuna haja wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO-19 kwa kuwa imeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kuwa ni salama kwa watu wote, wakiwamo wenye magonjwa ya muda mrefu.Angalizo hilo lilitolewa jana wakati wa semina kwa wanahabari na watu mashuhuri kuhusu afua za kinga dhidi ya tishio la wimbi la nne la UVIKO-19 na uhamasishaji wa chanjo hiyo iliyofanyika kwa njia ya mtandao.Profesa wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Deodatus Kakoko, alisema kuwa wajawazito hawakushirikishwa kwenye majaribio ya dawa, taarifa za usalama wao bado zinafanyiwa utafiti ingawa wajawazito  wameonekana kuwa katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo, hivyo waendelee kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyokuwa na maana.Prof. Kakoko alisema hakuna tatizo kwa kinamama wanaonyonyesha kupata chanjo ya UVIKO-19 na anashauriwa kuendelea kunyonyesha vyema hata kama amepata chanjo hiyo.Mtaalamu huyo wa afya pia alisema mgonjwa mwenye kisukari na mwenye Virusi vya Ukimwi (VVU) anaweza kupata chanjo hiyo kwa sababu inaongeza kinga mwilini na inaweza kumsaidia kuongeza kinga na kupunguza kabisa maambukizi hayo.Prof. Kakoko aliwataka vijana wanaosambaza taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii juu ya chanjo hiyo, waache mara moja kwa kuwa kwa sasa serikali inaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na itakapomaliza ilhali uvumi ukiendelea, wataanza kuchukuliwa hatua za kisheria."Mwanzo wizara ilitaka kuanza kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanavumisha taarifa za chanjo, tukashauri tuendelee kutoa elimu kabla ya kuanza kuwachukulia hatua, hivyo ninawataka vijana waache na wajitokeze kupata chanjo hii kwa sababu wao ndio taifa la kesho," alisema Prof. Kakoko.Katika mkutano huo wa mtandaoni, Mchungaji Daniel Mgogo, aliwataka viongozi wenzake wa kiroho kuepuka mahubiri yenye lengo la kupotosha kuhusu chanjo ya corona badala yake wajikite kwenye taarifa sahihi zinazotoka kwa wataalamu wa afya. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliwataka waandishi wa habari kutumia vyema kalamu zao kufikisha elimu ya umuhimu wa chanjo ya corona kwa wananchi ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 nchini.Msigwa alisema msimamo wa sasa wa serikali dhidi ya COVID-19 ni kujikita kwa maelekezo ya wataalamu wa afya na si vinginevyo.

Habari Kubwa