Watafiti wabaini miti 10 inayotibu corona

21May 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Watafiti wabaini miti 10 inayotibu corona

TAASISI ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori), imebaini miti 10 ambayo ina uwezo wa kutibu dalili za awali za mtu ameambukizwa virusi vya corona.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Misitu Tanzania (TAFORI), Revocatus Mushumbusi (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la uhifadhi wa misitu, mkoani Shinyanga jana, kuhusu taasisi hiyo kubaini miti 10 yenye uwezo wa kutibu dalili za awali za mtu mwenye maambukizo ya virusi vya corona. PICHA: MARCO MADUHU

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Revocatus Mushumbusi, aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga kwenye eneo la uhifadhi wa misitu.

Alisema wamebaini miti 10 ambayo ina uwezo wa kutibu dalili za awali za mtu mwenye maambukizo ya virusi hivyo vilivyotikisa dunia tangu vilipogungulika Desemba mwaka jana Wuhan, China.

Mushumbusi alisema miti ya asili ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na janga hilo kwa ama kujifukiza au kunywa maji yake yaliyochanganywa na mizizi ambayo inatibu dalili za awali, ikiwamo homa kali, kikohozi, mafua, kichwa, kifua kubana na kushindwa kupumua.

“Wakati dunia nzima inapambana na ugonjwa wa corona ambao bado haujapata dawa wala chanjo, na kinachotibika ni dalili zake, Taasisi ya Utafiti wa Misitu tunaamini kuwa kupitia miti hii 10 ya asili ambayo imekuwa ikitibu dalili za magonjwa kama hayo ya corona, wananchi wakiitumia ipasavyo watakuwa salama.

“Miti hii 10 ni Mlungulungu, Nengo Nengo, Mwatya, Mlundalunda, Mfutwambula, Ningiwe, Mgada, Mondo, Msana, Mlungulungu, na Mzima, ambapo mizizi na majani yake, yamekuwa yakitibu magonjwa mbalimbali ambayo yana dalili zote za awali za mtu mwenye maambukizo ya virusi vya corona,” alisema.

Alitaja baadhi ya magonjwa ambayo yanatibika kwa kutumia miti hiyo ya asili kuwa ni homa kali, kikohozi, mafua, kichwa, homa ya mapafu, matatizo ya tumbo, kifua, ganzi, malaria, athma, kuharisha, upungufu wa damu, ugumba, kibofu cha mkojo, vidonda vya koo na kushindwa kupumua.

Mtaalamu wa tiba za asili mkoani Shinyanga, Mussa Kuhaghaika, alisema tiba hizo zimekuwa zikisaidia katika kipindi hiki cha Janga la maambukizo ya corona na watu wamekuwa wakijifukiza na kunywa, huku akitoa wito kwa serikali kuendelea kufanya utafiti wa tiba hizo asili, akimini huenda zikawa dawa ya corona.

Habari Kubwa