Wataka kutambuliwa siku ya watu maskini

25Oct 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Wataka kutambuliwa siku ya watu maskini

MWANAHARAKATI wa watu maskini, Venance Magombera, ameitaka serikali na wananchi kuitambua na kuisherehekea siku ya watu wanaoshi kwenye umaskini uliopindukia.

Hatua hiyo ni sehemu ya kuwafariji na kuunganisha nguvu za namna ya kuwakomboa kiuchumi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Magombera, ambaye ni kiongozi wa Taasisi ya Organized by all together in Dignity (ATD), alisema kutokana na shughuli za kuwainua maskini wamefanikiwa kuunda vikundi vya wanawake ambao wanafanya ujasiriamali unaowakomboa kwenye hali duni.

Alisema wanatarajia kuwa na maonyesho ya bidhaa zinazotengenezwa na watu wa hali duni yatakayofanyika Jumapili eneo la Alliance Francaise, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupunguza umaskini, ambayo kwa Tanzania huadhimishwa Oktoba 17 kama siku ya watu fukara.

Vikundi hivyo ni wanawake wanaopinga umaskini cha Iloganzara (IWAPOA) na wanawake wajasiriamali wa Tandale, Boko na Tegeta (TABOTE), ambao wanajishughulisha na kugonga kokoto kupata kipato na sasa wanafanya ujasiriamali wa kutengeneza sabuni mbalimbali ili kujipatia kipato kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ufaransa nchini.

“Kila siku tunasikia siku ya jambo fulani, kila Oktoba 17 ni siku ya watu maskini lakini hakuna anayeipa kipaumbele, umaskini ni mgumu sana mnavyotuona hapa tunatwanga kokoto usiku na mchana kuweza kutoka kwenye hiyo hali kwa kufanya ujasiriamali ni hatua kubwa sana, tunashukuru Ufaransa kwa kuendelea kutuwezesha miradi midogo midogo ya kuwainua watu wa hali duni,” alisema Magombera.

Habari Kubwa